Mkutano wa Xi Jinping, Kim Jong-Un na Putin wamkera Trump
BEIJING, CHINA
RAIS Xi Jinping wa China Jumanne alikutana na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un jijini Beijing katika hatua inayoonyesha mshikamano wa mataifa yanayokinzana na Magharibi.
Haya yanajiri huku dunia ikitazama kwa makini athari za ushirikiano huu mpya wa kijeshi na kiuchumi.
Ni mkutano ambao umemchemsha Rais wa Amerika Donald Trump huku akielezea hisia kali kwenye mtandao wake wa Truth Social.
Aliandika: “Swali kubwa ambalo bado halijajibiwa ni ikiwa Rais Xi wa Uchina atataja msaada mkubwa na damu ya Waamerika wakati wa vita vyao vya ukombozi. Waamerika wengi walikufa na natumai watakumbukwa kwa kujitoa mhanga kusaidia China. Kuweni na sherehe njema. Na tafadhali, wape salamu zangu Vladimir Putin na Kin Jong Un wakati mnapopanga kudhuru Amerika.”
Xi alifanya mazungumzo na Putin hadharani na baadaye nyumbani kwake binafsi, akimrejelea kiongozi huyo wa Urusi kama ‘rafiki yake’.
Baada ya muda mchache, treni ya kivita ya Kim ilishuhudiwa ikiingia Beijing, huku vyombo vya habari vya Korea Kaskazini vikithibitisha kwamba kiongozi huyo alikuwa ameambatana na binti yake, Kim Ju Ae, anayechukuliwa na idara za kijasusi za Korea Kusini kama mrithi wake wa kisiasa.
Jumanne, viongozi hao watatu wanatarajiwa kushiriki kwenye gwaride kubwa la kijeshi jijini Beijing, tukio litakalodhihirisha ujasiri wa Xi katika kutangaza mpangilio mpya wa dunia wakati ambapo sera za Rais wa Amerika, Donald Trump zinavuruga mshikamano wa Magharibi.
Zaidi ya njiwa 80,000 wanatarajiwa kuachiliwa kupaa angani huku maelfu ya wananchi wakishuhudia vifaa vya kisasa vya kijeshi vikionyeshwa kwa fahari.
Wataalamu wa masuala ya usalama wanasema ushirikiano wa karibu kati ya Beijing, Moscow na Pyongyang unaweza kubadili mizani ya nguvu za kijeshi katika eneo la Asia na Pasifiki.
Hii inatokana na makubaliano ya kijeshi yaliyosainiwa kati ya Urusi na Korea Kaskazini mwaka 2024 na ushirikiano unaokua kati ya Pyongyang na Beijing.
Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari akiwa Beijing, Rais Putin alisema kwamba serikali ya Rais Trump “inasikiliza hoja za Urusi” kuhusu vita vya Ukraine.
Alidai kuwa sasa Moscow na Washington zimefikia “maelewano ya pamoja” kuhusu mzozo huo, ingawa hakutoa maelezo ya kina.
Hata hivyo, Trump amewahi kuonya kwamba endapo Urusi haitaonyesha ushirikiano katika juhudi za amani zinazoongozwa na Washington, inaweza kukabiliwa na “adhabu kali”.
Wakati wa mkutano huo, kampuni ya nishati ya Urusi, Gazprom, na Shirika la Petroli la Kitaifa la China (CNPC) zilisaini makubaliano ya kuongeza kiwango cha gesi kitakachosafirishwa China na kujenga bomba jipya litakalosambaza nishati kwa miaka 30 ijayo.
China ilionyesha kwa mara ya kwanza nguvu zake za kijeshi kupitia kwa nuclear triad (nyuklia ya angani, ardhini na baharini) inayojumuisha makombora ya masafa marefu (ICBMs), ndege zisizo na rubani za torpedo, silaha za kasi ya hypersonic pamoja na vifaru vipya vya kivita aina ya Type-100, vyote hivi vikiwa sehemu ya gwaride kubwa zaidi kuwahi kufanyika nchini humo.
Onyesho hilo lilichukuliwa kama ujumbe wa wazi kwa mataifa ya Magharibi kuhusu kiwango cha nguvu ya kijeshi ya Beijing.
Katika hotuba yake wakati wa gwaride, Rais Xi Jinping alisema dunia kwa sasa iko katika njia panda kati ya “amani na vita”.
Alisisitiza kuwa maonyesho hayo ya kijeshi ni tangazo la wazi kuhusu mpangilio mpya wa dunia unaojengeka na kwamba China iko tayari kulinda maslahi yake kwa nguvu zote.
Wakati huo huo, mazungumzo yasiyokusudiwa kusikika baina ya Putin na Xi yalinaswa na kipaza sauti kilichokuwa wazi.
Katika mazungumzo hayo walijadili masuala ya kibayoteki, ikiwemo upandikizaji wa viungo na uwezekano wa maisha marefu zaidi ya karne moja, huku Xi akieleza matarajio kwamba mwanadamu anaweza kufikia umri wa miaka 150 katika siku zijazo.
Kwa upande mwingine, Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, aliahidi kumuunga mkono Rais Putin “kwa kila njia iwezekanavyo” na kumpongeza hadharani kwa mshikamano wao.
Baada ya mazungumzo yao yaliyodumu takribani saa mbili na nusu jijini Beijing, Kim alimkumbatia Putin kama ishara ya urafiki wa dhati na mshikamano wa kijeshi.
Putin naye alimshukuru Kim kwa msaada wa taifa lake katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine.
Alimualika kiongozi huyo wa Korea Kaskazini kufanya ziara nyingine ya kikazi nchini Urusi, akisema ushirikiano wao unaendelea kukua na kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kisiasa na kijeshi kati ya mataifa hayo mawili.