Mnyarwanda aishtaki UG, adai Sh100m kwa mateso
Na IVAN MUGISHA
MWALIMU raia wa Rwanda anayedaiwa kukamatwa na kuteswa nchini Uganda amewasilisha kesi katika Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki akitaka alipwe fidia ya Sh100 milioni (dola 1 milioni).
Kesi hiyo, hata hivyo, huenda ikasababisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya Rwanda na Uganda kudorora zaidi.
Mataifa hayo mawili jirani yamekuwa yakizozana kwa miezi mitatu sasa na uhasama huo umeathiri zaidi shughuli za kibiashara na usafiri.
Bw Venant Hakorimana aliwasilisha kesi katika mahakama hiyo iliyoko mjini Arusha, Tanzania Jumatatu kupitia kwa wakili wake Richard Mugisha.
Hakorimana, 35, aliambia Taifa Leo kuwa alikamatwa mnamo Julai mwaka jana mara tu baada ya kuwasili jijini Kampala, Uganda na akawekwa kizuizini kwa miezi kumi.
Alidai kuwa aliteswa na maafisa wa usalama alipokuwa gerezani nchini Uganda.
“Nilikuwa mwalimu wa Biolojia nchini Ethiopia. Nilikamatwa mwaka jana nilipoenda nchini Uganda kukagua mali yangu wilayani Mbarara,” akasema Bw Hakorimana.
Alisema maafisa wa usalama wa Uganda walimpiga kila siku na hata kumchoma kwa nyaya za umeme.
Hatia
Alisema kuwa baada ya kuishi gerezani kwa miezi tisa alifikishwa mahakamani ambapo alikutwa na hatia ya kuingia nchini humo bila kibali na akahukumiwa kifungo cha miezi 12 gerezani au faini ya Sh26,600.
Alilipa faini na kisha akarejeshwa makwao kwa nguvu na serikali ya Uganda.
Mwalimu huyo atawakilishwa bila malipo na wakili maarufu nchini Rwanda, Richard Mugisha, kudai fidia hiyo.
Bw Hakorimana ni raia wa tatu wa Rwanda kushtaki serikali ya Uganda kwa madai ya kuteswa na kuzuiliwa kinyume cha sheria.
Bw Ezekiel Muhawenimana namkewe Esperance Dusabimana walikamatwa na kushtakiwa katika mahakama ya Uganda na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kuingia nchini humo kiharamu kupitia mpaka wa Cyanika mnamo Agosti, 2018.
Walifungwa na kuachiliwa huru baada ya kutumikia kifungo kwa miezi tisa. Wameshtaki serikali ya Uganda na wanataka kulipwa fidia ya Sh10 milioni. Wawili hao pia wanawakilishwa na Bw Mugisha.
Mnamo Aprili, wakili wa Uganda Steven Kalali, aliwasilisha kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki akishutumu Rwanda kwa kuzuia biashara huru kufuatia hatua yake ya kufunga mpaka wa Gatuna Februari 2019.
Wiki iliyopita, Rwanda ilifungua mpaka wa Gatuna kwa siku 10 ili kufanyia majaribio miundomsingi mipya iliyowekwa.
Hata hivyo, bidhaa kutoka Uganda zinaendelea kuzuiliwa mpakani hapo.