Morsi azikwa katika mazingira ya ulinzi mkali
Na AFP
RAIS wa zamani wa Misri Mohamed Morsi alizikwa Jumanne majira ya asubuhi mashariki mwa Cairo, siku moja baada ya kuzimia mahakamani na kufariki baadaye.
Morsi alizikwa katika eneo la Madinat Nasr na familia yake iliruhusiwa kuhudhuria mazishi hayo, kulingana na mwanawe Ahmed Morsi.
Ahmed Morsi alisema serikali iliwakataza kusafirisha mwili hadi nyumbani kwa Morsi mkoani Sharqiya, Nile Delta.
“Tulioshea maiti katika hospitali ya gereza la Tora, tukamsomea sala ya mwisho hospitalini hapo kabla ya mazishi,” akasema.
Wakili wa Morsi, Abdel Moneim Abdel Maksoud, alithibitisha kuwa mwili wa mteja wake ulizikwa katika makaburi ya umma ya Al-Wafaa Wa al-Amal.
Morsi ambaye alikuwa kiongozi wa kundi la Muslim Brotherhood alikuwa kiongozi wa kwanza nchini Misri kuchaguliwa kidemokrasia mnamo 2012.
Alimrithi Hosni Mubarak aliyeng’olewa mamlakani kupitia mapinduzi baada ya kutawala Misri kwa miaka 30.