• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Mtakuja kuelewa umuhimu wa kubariki mashoga – Papa

Mtakuja kuelewa umuhimu wa kubariki mashoga – Papa

NA MASHIRIKA

VATICAN CITY, VATICAN

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amesema katika mahojiano yaliyochapishwa Jumatatu kwamba Waafrika ni ‘spesheli’ hasa katika uamuzi wake wa kuruhusu makasisi wa kanisa hilo kuwabariki mashoga.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alisema ana imani kuwa, isipokuwa Waafrika, wakosoaji wa uamuzi wake wa kuruhusu baraka kwa wapenzi wa jinsia moja, ulimwengu hatimaye utakuja kuielewa uamuzi huo.

Baraka ziliruhusiwa mnamo Desemba 2023 katika waraka uitwao Fiducia Supplicans (Supplicating Trust), ambao umezua mjadala mkubwa katika Kanisa Katoliki, huku upinzani mkali ukitoka kwa maaskofu wa Kiafrika.

“Wale wanaopinga vikali ni wa vikundi vidogo vya itikadi kali,” Papa Francis aliambia gazeti la Italia La Stampa.

“Kesi maalum ni Waafrika. Kwao ushoga ni kitu ‘kibaya’ kutoka kwa mtazamo wa kitamaduni,” akaongeza Papa Francis.

“Lakini kwa ujumla, ninatumai kwamba hatua kwa hatua kila mtu ataunga mkono tamko la ‘Fiducia Supplicans’ na kitengo cha Nguzo ya Imani ambacho lengo lake ni kujumuisha watu,” Papa alisema.

Wiki iliyopita, Papa Francis alionekana kukiri kuwa tamko lake lilikataliwa Afrika ambapo baadhi ya maaskofu wameukataa uamuzi wa kuwabariki mashoga na wapenzi wengine wa jinsia moja.

Alisema kwamba baraka zinapotolewa, makasisi wanapaswa “kwa kawaida kuzingatia muktadha, hisia, mahali anapoishi na njia zinazofaa zaidi za kufanya hivyo.”

Tangu Papa Francis alipotoa agizo hilo, viongozi tofauti wa kanisa wameeleza na kutoa hisia tofauti, baadhi wakijitokeza wazi kulipinga.

Kuvutia washiriki

Ingawa lengo kuu la agizo hilo linaonekana kama njia ya kuwavutia washiriki zaidi na kutowabagua watu hao, wachambuzi na wasomi wa masuala ya dini wanasema huenda agizo hilo lilitolewa bila Papa kupewa ushauri wa kina na uongozi wa kanisa hilo.

Kanisa Katoliki lina mamilioni ya washiriki hapa Kenya na barani Afrika kwa jumla.

Kulingana na takwimu kutoka kwa serikali, kanisa hilo ndilo linaloongoza kwa kuwa na washiriki wengi nchini, huku likifuatwa na makanisa ya Kiprotestanti.

Akigusia mapigano kati ya Israeli na Wapalestina, Papa Francis alisema ‘amani ya kweli’ kati yao haitapatikana hadi serikali za nchi hizo mbili kuamua kushirikiana.

Kando na hayo, Papa Francis alithibitisha kuwa ameratibiwa kukutana na rais wa nchi yake ya asili ya Argentina, Javier Milei, Februari 11, na kwamba hatimaye kuzuru nchi hiyo – ambako hajarejea tangu kuwa papa mwaka 2013 – ni jambo linalowezekana.

Alisema ajenda yake ya 2024 kwa sasa inajumuisha safari za Ubelgiji, Timor Mashariki, Papua New Guinea, na Indonesia.

  • Tags

You can share this post!

Supkem: Waislamu eneo la Pwani wamuunga Ole Naado

Nyong’o asifu mpango wa ujenzi wa SGR hadi Kisumu

T L