Kimataifa

Muafaka watikisika Israel ikiua 25 Gaza

Na NA REUTERS November 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

GAZA, PALESTINA

ZAIDI ya raia Wapalestina 25 waliuawa kwenye mashambulizi manne yaliyotekelezwa na Israel katika Ukanda wa Gaza Jumatano.
Mashambulizi hayo yalitekelezwa katika maeneo ambayo yanasimamiwa na Hamas.
Serikali ya Israel na wapiganaji wa Hamas walikuwa na mkataba wa kusitisha vita lakini mashambulizi hayo sasa yanaibua shaka iwapo ahadi ya kutopigana itadumishwa.
Israel ilisema ilishambulia Hamas baada ya wapiganaji hao kuwavamia wanajeshi wake ingawa hakuna mwanajeshi ambaye alikufa wakati wa shambulizi hilo.
Hamas ilikashifu mashambulizi ya Israel na ikaitaka Amerika iishinikize iheshimu mkataba wa Oktoba.
Hata hivyo, afisa mmoja kutoka Amerika alilaumu Hamas akisema kundi hilo linataka kukiuka makubaliano ya kusitisha vita ili lisipokonywe silaha.
“Hizi ni mbinu zao na hazitafaulu,” akasema afisa huyo.
Takwimu kutoka kwa madaktari zilisema kuwa watu 10 waliuawa eneo la Zeitoun viungani kwa jiji la Gaza.
Wengine wawili waliuawa Shejaja nao wengine wawili Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Mapigano ya mara kwa mara yamedaiwa kufanya iwe vigumu kuheshimu mkataba wa kusitisha vita.
Mkataba huo wenye hoja 20, uliafikiwa kutokana na shinikizo za Rais wa Amerika Donald Trump.
Mkataba huo ulioafikiwa Oktoba 10 baada ya vita vikali vya miaka miwili, pia umesababisha Wapalestina warejee nyumbani kwao.
Israel nayo iliwaondoa wanajeshi wake kwenye jiji la Gaza na kuruhusu misaada iwafikie Waplestina.
Israel inasema kuwa wanajeshi wake watatu wameuawa tangu mkataba huo ukumbatiwe na bado inawalenga wapiganaji wa Hamas.