Kimataifa

Mugabe aitwa bungeni kufichua yalikoenda mabilioni ya almasi

May 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

AFP na VALENTINE OBARA

HARARE, ZIMBABWE

KAMATI ya bunge la Zimbabwe imemwamuru rais wa zamani Robert Mugabe aende kutoa ushahidi Jumatano kuhusu sakata ya ufisadi wa almasi ambayo imedaiwa ilisababisha hasara ya mabilioni ya madola alipokuwa mamlakani.

Mugabe ambaye aliondolewa mamlakani kupitia kwa mapinduzi ya kijeshi Novemba mwaka uliopita hajasema kama atafika mbele ya kamati hiyo ambayo ilitoa notisi yake Jumatatu.

Rais huyo wa zamani aliye na umri wa miaka 94 ambaye huugua, alihitajika pia kutoa ushahidi wake mwezi uliopita lakini mkutano huo ukaahirishwa.

Wabunge wamepanga kumuuliza maswali kuhusu madai aliyotoa mwaka wa 2016 kwamba nchi hiyo ilipoteza dola bilioni 15 kwa ufisadi na wizi wa almasi zake kwa mataifa ya kigeni.

Hapakuwa na yeyote katika afisi ya Mugabe kuthibitisha kama atatii wito huo.

Mugabe hajaonekana hadharani tangu Novemba ingawa alifanya karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa kwake Februari nyumbani kwake ambako anaishi na mke wake Grace, mwenye umri wa miaka 52.

Nafasi yake ya uongozi ilitwaliwa na aliyekuwa naibu wake, Emmerson Mnangagwa, ambaye aliungwa mkono na maafisa wakuu wa kijeshi.