Museveni ashida seven-tam, Bobi akihepa jeshi huku UN ikisema kura ilijaa vitisho na dhuluma
KAMPALA, UGANDA
RAIS Yoweri Museveni amechaguliwa tena kwa muhula wa saba, Tume ya Uchaguzi ya Uganda ilitangaza jana.
Museveni, 81, alizoa asilimia 71.65 ya kura hiyo iliyopigwa Alhamisi ambayo ilitarajiwa pakubwa angeshinda.
Alimshinda mpinzani wake mkuu mwanasiasa na mwanamuziki Bobi Wine ambaye alizoa kura asilimia 24.72, kulingana na matokeo rasmi.
Ushindi wa Museveni unafuatia kampeni zilizoghubikwa na mivutano na malalamishi tele.
Umoja wa Mataifa (UN) ulisema mchakato wa uchaguzi ulisheheni “ukandamizaji na vitisho vingi”, dhidi ya mikutano ya upinzani.
Kuelekea uchaguzi maafisa wa polisi na jeshi walivuruga mikutano ya upinzani kwa vitoa machozi na nguvu kupita kiasi, hali iliyozua hofu miongoni mwa wapiga kura.
Aidha, kulikuwa na madai ya kukamatwa kwa wanaharakati, kudhibitiwa kwa uhuru wa kujieleza na kuzimwa kwa mtandao wa intaneti siku ya kura na wakati wa kuhesabiwa kwa matokeo.
Bobi Wine, 43, ambaye alikuwa akiwania urais kwa mara ya pili, amepinga matokeo hayo akidai yamejaa udanganyifu na yaliingiliwa na idara za serikali.
Hata hivyo, tume ya uchaguzi imesisitiza kuwa zoezi hilo lilifanyika kwa mujibu wa sheria.
Mapema jana polisi nchini Uganda walikanusha madai kuwa Wine alitekwa nyara Ijumaa jioni huku chama cha mgombeaji huyo National Unity Platform (NUP) kikisema helikopta ya kijeshi ilitua katika uwanja wenye makazi yake jijini Kampala na wanajeshi wakamchukua kwa nguvu wakampeleka kusikojulikana.
Hata hivyo, baadaye kiongozi huyo wa upinzani alitoa taarifa akisema kwamba alifanikiwa kutoroka wakati wa uvamizi wa usiku uliofanywa na vikosi vya usalama, ingawa mke wake na jamaa wengine bado wanazuiliwa nyumbani.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari Jumamosi asubuhi, msemaji wa polisi Kituuma Rusoke alisema Bobi Wine bado alikuwa nyumbani kwake, akidai kuwa ni wanafamilia wake waliokuwa wakisambaza taarifa “zisizo za kweli na zisizo na msingi.”
“Tumedhibiti maeneo yanayochukuliwa kuwa hatari kwa usalama. Hatuwezi kuruhusu watu kutumia maeneo fulani kukusanyika na kusababisha vurugu,” alinukuliwa akisema na gazeti la Daily Monitor la Uganda.
Alisisitiza kuwa hatua za polisi zililenga kuzuia ghasia au juhudi za kuyumbisha usalama wa nchi.
Wakati huo huo, mwanawe Bobi Wine, Solomon Kampala, alichapisha ujumbe mitandaoni akikiri kuwa alikuwa akipokea taarifa zinazokinzana kuhusu hali ya usalama katika makazi ya wazazi wake.
Changamoto ya upatikanaji wa intaneti imefanya iwe vigumu kuthibitisha taarifa zinazozagaa.
Mnamo Jumamosi mchana, Bobi Wine aliandika ujumbe kwenye Facebook akieleza kuwa hali ilikuwa “ngumu sana” nyumbani kwake katika eneo la Magere, Kampala, usiku wa Ijumaa.
Alidai kuwa wanajeshi na polisi walivamia makazi hayo, wakakata umeme na kuharibu baadhi ya kamera za CCTV huku helikopta zikizunguka juu.
“Ninathibitisha kuwa nilifanikiwa kutoroka. Kwa sasa siko nyumbani, ingawa mke wangu na wanafamilia wengine bado wanazuiliwa,” alisema, akiongeza kuwa kuzimwa kwa intaneti kote nchini kumechochea uvumi mwingi.
Bobi Wine alisisitiza kukataa kwake matokeo ya uchaguzi, akidai kulikuwa na wizi wa kura, jeshi kuingilia uchaguzi, na kukamatwa kwa viongozi wa chama chake na maafisa wa uchaguzi.
Ghasia ziliripotiwa ikisemekana kuwa angalau wafuasi saba wa upinzani waliuawa katika mazingira tata.
Ubalozi wa Amerika pia ulitoa tahadhari kwa raia wake kufuatia madai ya matumizi ya gesi ya kutoa machozi na ufyatuaji wa risasi hewani na vikosi vya usalama.
Ripoti nyingine zilisema watu 12 waliuawa baada ya kushambuliwa kwa risasi na polisi nyumbani kwa mgombeaji wa ubunge wa upinzani.