Kimataifa

Museveni pazuri kushinda muhula wa saba licha ya kampeni kali za Bobi Wine

Na MASHIRIKA January 13th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

KAMPALA, Uganda

RAIS wa Uganda Yoweri Museveni anatarajiwa kuendeleza uongozi wake wa miongo minne kwa kushinda katika uchaguzi mkuu ulioratibiwa kufanyika Alhamisi wiki hii.

Kiongozi huyo, aliyeingia mamlakani kwa njia ya mapinduzi mnamo 1986, anakabiliwa na wapinzani saba katika uchaguzi huo.

Museveni, 81, anasema miaka minne uongozini, muhula wake wa saba, itampa nafasi ya kulinda manufaa yaliyopatikana nchini Uganda na uongozi wake ulioleta amani na uthabiti.

Mpinzani mkuu miongoni mwa wapinzani hao ni Bobi Wine, ambaye zamani alikuwa mwanamuzi wa mtindo wa Pop kabla ya kujiungana siasa.

Katika uchaguzi wa urais wa 2021, Bobi Wine, 43, alipata asimilia 35 ya kura na ameibua msisimko mkubwa miongoni mwa wapigakura vijana wanaolalamikia shida ya ukosefu wa ajira na kukithiri kwa ufisadi.

Rais Museveni ameifanyia mageuzi Katiba ya Uganda mara mbili kuondoa hitaji la umri na lile la kumtaka rais kuongoza kwa mihula mahsusi.

Kiongozi huyo pia amedhibiti taasisi zote nchini Uganda hali inayoashiria kuwa itakuwa vigumu kuondolewa kwake mamlakani kupitia kura, wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanasema.

Lakini uchaguzi wa Alhamisi na fujo zozote zitakazokumba upigaji kura, zitakuwa ni mtihani muhimu kwa nguvu zake za kisiasa, miaka minne baada ya Amerika kudai uchaguzi uliopita haukuendeshwa kwa njia huru na haki.

Uganda ni mshikadau muhimu katika siasa za Afrika Mashariki na wanajeshi wake wametumwa kudumisha amani katika nchi za Somalia, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Equatorial Guinea.