Muumini aishi na maiti ya pasta nyumbani miezi miwili akisubiri afufuke
POLISI nchini Tanzania, wanamzuilia mwanamke mmoja aliyekamatwa kwa kuhifadhi mwili wa pasta wa kanisa lake kwa miezi miwili ndani ya nyumba akisubiri afufuke.
Katika tukio lililowaacha wakazi wa Wadi ya Kalenga, mkoani Iringa wakiwa wamepigwa butwaa, muumini wa Kanisa la El-Huruma (EHC), Agnes Mwakijale alikamatwa kwa kuuhifadhi nyumbani kwake kwa miezi miwili, mwili wa mchungaji wake John Chida uliokuwa ukioza.
Inasemekana kwamba Mchungaji Chida aliaga dunia mapema Oktoba 2024, lakini kifo chake kilijulikana Desemba 3, wakati mwenyekiti wa kijiji cha Isakalilo ‘C’ Bw Amos Msole alipogundua mwili huo.
Mabaki ya pasta huyo mwenye umri wa miaka 70 yalikuwa yameoza kwa kiasi kikubwa, na kuacha uvundo usiovumilika ambao ulisababisha maafisa wa eneo hilo kuchukua hatua.
Bw Msole alieleza kuwa wasiwasi ulitanda baada ya wakazi kuripoti hali mbaya ya kiafya ya mchungaji huyo mwezi Oktoba lakini hawakujua aliko.
“Nilisimama karibu na nyumba wakati nikirudi kutoka shambani kwangu ili kumjulia hali mchungaji kwa sababu nilijua alikuwa mgonjwa. Nilimuuliza yule mama [aliyekuwa pale nyumbani] kumhusu, akasisitiza kuwa ‘amepumzika.’ Nilikuta mwili ukiwa umeoza, uvundo haukuweza kuvumilika,” alisema.
Alipoulizwa kwa nini hakuripoti kifo hicho, Agnes alieleza kwamba kasisi huyo alikuwa ametangaza kwamba “atapumzika kwa muda” kabla ya kufufuka.
Aliamini unabii huo na akaendelea kutunza mabaki yake, akiusafisha mwili wake, akibadilisha nguo, na kuutunza kana kwamba alikuwa hai.
Msole alibainisha zaidi kuwa Mchungaji Chida alikuwa akiishi kwa kujitenga tangu awasili kijijini Isakalilo C na kuanzisha tawi la Kanisa la El-Huruma mnamo 2022.
Baada ya safari aliyofanya Mwanza katikati ya mwaka wa 2024, afya yake ilianza kudhoofika, lakini alikataa msaada wa matibabu, akisisitiza kwamba Mungu angeingilia kati na kumponya.
Kuchelewa kugunduliwa kwa mwili wake kulitokana tabia yake ya kutotangamana sana na majirani.
Polisi wa Mkoa wa Iringa walifahamishwa na mwili ukahamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
Mkuu wa hospitali hiyo Dkt Alfred Mwakalebela, alithibitisha kuwa mabaki hayo yalikuwa katika hali ya kuharibika.
Mwanasaikolojia wa eneo hilo, Leonard Mgina, alisema kuwa tabia ya Agnes iliashiria dhiki inayoweza kutokea ya kisaikolojia au hamasa kubwa ya kidini, na kupendekeza tathmini ya kiakili inaweza kuwa muhimu.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allen Bukumbi kwa maelezo zaidi hazikufua dafu.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa, na uchunguzi unaendelea.