Muungano wa Ulaya wateta kuhusu upinzani kuteswa Tanzania
Na AFP
NAIROBI, KENYA
MUUNGANO wa Ulaya (EU) umeonya kuwa ghasia zilizoshuhudiwa hivi majuzi nchini Tanzania zinaweza kuhatarisha demokrasia katika nchi hiyo.
“Tunasema kwa masikitiko kwamba matukio ya hivi majuzi nchini Tanzania ni tishio kwa demokrasia na haki za Watanzania,” EU ilisema katika taarifa Ijumaa.
Muungano huo ulisema kwamba unahuzunishwa na kupigwa risasi kwa mwanafunzi kwenye mkutano wa kisiasa wa upinzani jijini Dar es Salaam mapema mwezi huu. Ulitaka uchunguzi wa kina wa vifo vyote vya wanasiasa na watetezi wa haki za binadamu hivi majuzi kufanywa.
“Tunasikitishwa na ongezeko la ghasia katika miezi ya hivi majuzi,” EU ilisema.
Mnamo Ijumaa chama cha upinzani cha Chadema kilisema kwamba afisa wake mmoja aliuawa akiwa kati kati ya nchi hiyo na kutaja mauaji hayo kama mauaji ya kisiasa.
Mnamo Septemba mwezi jana, mbunge wa upinzani Tundu Lissu alinusurika baada ya kupigwa risasi kadhaa akiwa nyumbani kwake jijini Dodoma.
Hivi majuzi, Amerika ilieleza wasiwasi kuhusu ghasia za kisiasa nchini Tanzania.