Mwanahabari ni miongoni mwa waliouawa kwenye ghasia Kabul
Na AFP
KABUL, Afghanistan
ALIYEKUWA mtangazaji wa runinga nchini Afghanistan na raia wawili wameuawa katika mlipuko wa bomu jijini Kabul, polisi wamesema, kuhusu ghasia za hivi punde kukumba jiji hilo.
Yama Siawash aliwauawa wakati bomu ambalo lilitegwa katika gari lake lililipuka karibu makazi yake, msemaji wa polisi Ferdaws Faramarz aliwaambia wanahabari.
Siawash, ambaye alijiunga na Benki Kuu nchini Afghanistan kuhudumu kama mshauri, aliwahi kufanya kazi kama mtangazaji wa kipindi cha kisiasa katika runinga ya Tolo News, ambayo ni kituo cha mmiliki binafsi.
Hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo.
Hata hivyo, watu mashuhuri, wakiwemo wanahabari, viongozi wa kidini, wanasiasa na wanaharakati wa kutetea haki, wamekuwa wakiuawa jijini Kabul na miji mingine katika msururu wa ghasia unaokumba nchi hiyo.
Tukio la kuuawa kwa Siawash limelaaniwa na maafisa wa ngazi za juu katika serikali ya Afghanistan.
“Kuwaua wanahabari ni sawa na kuhujumu uhuru wa uanahabari na kujieleza na kifo cha Siawash ni pigo kubwa kwa nchi yetu,” Abdullah, ambaye anaongoza mpango wa amani na maridhiano alisema kwenye taarifa.
Akaongeza: “Huu ni uhalifu ambao hauwezi kukosa kuadhibiwa na hauwezi kusahauliwa.”