Mwanamume achapwa viboko msikitini kwa kupatwa na mwanamke
KUALA LUMPUR, MALAYSIA
MWANAUME mmoja Ijumaa alicharazwa viboko kwenye msikiti mmoja kaskazini mashariki mwa jimbo la Terengganu kutokana na kosa la kupatikana akiwa na mwanamke mwengine pekee yake katika eneo la siri.
Mohd Affendi Awang, 42, aliadhibiwa kutokana na kosa hilo linalofahamika kama ‘khalwat’ kwenye dini ya Kiislamu. Aliadhibiwa kwa kucharazwa viboko sita baada ya kikiri kosa hilo mwezi uliopita.
‘Khalwat’ ni sheria ambayo inazuia mwanaume kupatikana na mwanamke ambaye si jamaa yake au bibi yake wakiwa wawili wamejificha kivyao.
Mara nyingi wanaopatikana wamejitenga na kujificha hushukiwa wana nia ya kushiriki mapenzi.
Affendi ambaye ni baba wa watoto watano alifanyiwa vipimo vya kimatibabu kabla ya kuchapwa viboko kwenye msikiti wa Terangganu.
Tukio hilo lilishuhudiwa na watu 90 na maafisa wa polisi ambao mmoja wao kutoka idara ya magereza ya jimbo hilo.
Alicharazwa viboko hivyo kwa dakika mbili. Jimbo la Terengganu linasimamiwa na sheria za Kiislamu.
Mnamo 2018, wanawake wawili walichapwa ndani ya korti huku watu wakitazama baada ya wao kupatikana na hatia ya kuwa wasagaji.
Kuchapwa kwao kulilaaniwa na makundi ya kupigania haki za kibinadamu.