Mwanamuziki nyota wa nyimbo za Country, Kenny Rogers afariki
Na MASHIRIKA
GEORGIA, AMERIKA
KENNY Rogers, nyota wa muziki aina ya Country na mshindi wa Tuzo za Grammy, amefariki akiwa na umri wa miaka 81.
“Rogers alifariki bila masumbuko mengi nyumbani kwake alikokuwa akitunzwa akiwa amezingirwa na familia yake,” ilisema taarifa kutoka kwa meneja wake wa mawasiliano Keith Hagan.
Kulingana na taarifa iliyochapishwa jana, alifariki nyumbani kwake Sandy Springs, Georgia.
“Kenny Rogers aliacha kumbukumbu ya kudumu katika historia ya muziki si nchini mwake Amerika tu bali duniani kote. Nyimbo zake zimevutia wapenzi wa muziki na kugusa maisha ya mamilioni ya watu kote ulimwenguni,” ilisema taarifa.
Familia ya Rogers inapanga ibada ya faragha kutokana na hofu kuhusu dharura ya kimataifa ya virusi vya corona.
Rogers alifahamika vyema kwa kibao chake kilichovuma sana The Gambler, kilichotolewa mnamo 1978. Vibao vingine maarufu alivyowahi kuchomoa ni pamoja na Coward of the County, The Vows go Unbroken, Lucille, We’ve Got Tonight, Lady, Islands In The Stream na Thoughts the Years.
Aliongoza chati ya wanamuziki bora katika miaka ya 1970 na 1980, na kushinda tuzo tatu za Grammy.
Aliwahi kuuza albamu milioni 50 nchini Amerika pekee. Aidha, aliwahi kuibuka mshindi katika makala sita ya Tuzo za Muziki wa Country.
“Muziki wa Country umepoteza gwiji Kenny Rodgers, ambaye ameacha taathira ya kudumu katika historia ya fani hii ya muziki,” Muungano wa Muziki wa Country ulisema kwa taarifa.
Amekuwa mwanamuziki wa fani hii kwa zaidi ya miongo sita. Alistaafu uimbaji mnamo 2015.
“Nimekuwa na bahati sana kudumu katika taaluma hii kwa muda mrefu kama huu mbali na kuwa na mashabiki wa dhati. Lakini huja wakati ambapo mtu anastahili kukaa na familia yake.”
“Maisha yangu kwa sasa yanahusu mke wangu na pacha wangu wa miaka 11. Kuna mambo mengi ambayo ningependa kufanya pamoja nao,” aliongeza wakati akitangaza kustaafu.