Mwanaume Mkenya kusota jela Amerika miaka 20 kwa kujilazimishia kimapenzi kwa ajuza, 70
MWANAUME Mkenya atakula maharagwe kwa miaka 20 katika gereza la Amerika kwa kumdhulumu kimapenzi ajuza, 70 mwaka jana.
Brian Kibiwot Chucheney alihukumiwa miaka 20 kutokana na kosa hilo dhidi ya mwanamke huyo ambaye alikuwa mpokezi katika jumba la karibu wanakoishi watu. Mwanasheria wa Maricopa Rachel Mitchell ndiye alitoa adhabu hiyo kali dhidi ya Kibiwot.
Tukio hilo lilifanyika wakati ambapo ajuza huyo alikuwa kwenye zamu ya usiku, Kibiwot alibisha dirisha la jumba hilo saa 10.30 usiku Jumapili akiomba msaada.
Ajuza huyo aliamini kuwa Kibiwot alikuwa akiishi kwenye jumba hilo na akamruhusu ndani. Akiwa ndani Kibiwot aliomba kuenda haja chooni kabla ya kuomba maji ya kunywa ndani ya chumba cha mwanamke huyo.
Alimfuata mwanamke huyo kisha akambaka na kuiba nguo za ajuza huyo kisha akahepa nazo. Polisi walimsaka Kibiwot na kumpata saa chache baada ya tukio hilo.
Polisi walisema kitendo cha Kibiwot kinaonyesha wazi kuwa yeye ni hatari kwa usalama wa jamii kwa sababu hata hakujutia kitendo chake.
“Nashukuru kazi safi ya Naibu Mwanasheria wa Kaunti Maren Soreson kwa sababu sasa atatumikia kifungo cha kipindi kirefu kutokana na kitendo chake,” akasema Mitchell.
Kibiwot alikiri mashtaka matatu yaliyokuwa yanamkabili, mmoja ya utekaji nyara na mengine mawili ya jaribio la dhuluma za kimapenzi. Kifungo cha miaka 20 ni kutokana na utekaji nyara kisha pia mienendo yake itakuwa ikifuatiliwa hata akitoka gerezani kuhakikisha hadhuru watu zaidi.
Mwanasheria huyo alisema kuwa kitendo cha Kibiwot kilimdhalilisha ajuza huyo na kumwacha na msongo wa mawazo pamoja na makovu tele maishani.
Pia kitendo hicho kilimharibia motisha ya kazi na kuathiri familia yake.
Ili kuepuka vitendo kama hivyo, kumetokea pendekezo kuwa usalama uimarishwe kwenye majumba na pia kuwe na mafunzo kuhusu dhuluma za kijinsia.