Mwanawe Gaddafi aachiliwa baada ya kuzuiliwa miaka 10 Lebanon
BEIRUT, LEBANON
HANNIBAL Gaddafi, mwana mdogo wa aliyekuwa Rais wa Libya, marehemu Muammar Gaddafi, aliachiliwa huru mnamo Jumatatu jioni baada ya kuzuiliwa nchini Lebanon kwa karibu miaka 10.
Alikuwa akizuiliwa bila hata kuruhusiwa kujitetea kutokana na kutoweka kwa Imam Musa al-Sadr, ambaye alikuwa kiongozi wa Waislamu wanaoegemea dhehebu la Shi’ite.
Imam Musa alitoweka kwa njia tata mnamo 1978 alipokuwa ziarani Libya na ujumbe wake, tukio ambalo lilizua uhasama mkubwa kati ya Lebanon na Libya.
Kipindi hicho, Hannibal alikuwa na umri wa miaka miwili pekee. Hata hivyo, utawala wa Lebanon haukujali hilo na ulimshutumu kwa kuficha habari kuhusu kutoweka kwa Imam Musa.
Hannibal alitekwa nyara mnamo 2015 na wapiganaji wa Syria ambako alikuwa akiishi uhamishoni na mkewe na watoto wake baada ya babake kuuawa kwenye maasi yaliyotokea Libya mnamo 2011.
Makundi ya haki za kibinadamu yalilalamikia kuhusu kuendelea kuzuiliwa kwa Hannibal na kusema mashtaka dhidi yake yalikuwa ya kubuniwa tu.
Mnamo 2023, Hannibal alishiriki mgomo wa kutokula gerezani akilalamikia kuzuiliwa kwake na hali yake ya kiafya iliyokuwa imedorora na alihitaji matibabu ya dharura.
Mwezi uliopita, Mahakama ya Lebanon iliamrisha waachiliwe huru tena kwa dhamana ya Sh1.4 bilioni.
Hata hivyo, mawakili wake walipinga dhamana hiyo wakisema ilikuwa juu mno. Baada ya kupambana mahakamani, ilipunguzwa hadi Sh1.1 bilioni na pia ikaondoa vikwazo ambavyo Hannibal alikuwa amewekewa.
“Aliachiliwa baada ya mawakili wake kulipa dhamana hiyo,” duru kutoka mahakama ambapo kesi yake ilikuwa ikisikizwa ikasema.
Serikali ya Libya chini ya Abdulhamid al-Dbeibah kutoka makao yake Tripoli ilishukuru uongozi wa Lebanon na spika wa bunge kwa kushirikiana kuhakikisha Hannibal anaachiliwa huru.