Kimataifa

Mwandishi akaangwa kudai wanawake wazee hawawezi kumsisimua kimahaba

January 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA na PETER MBURU

MWANDISHI mmoja kutoka Ufaransa amekashifiwa vikubwa kufuatia matamshi yake kuwa hawezi kupenda wanawake walio na umri wa zaidi ya miaka 50, kwa kuwa ‘ni wazee sana’.

Bw Yann Moix alieleza gazeti moja la taifa hilo kuwa wanawake wa umri huo ni wazee sana na kuwa miili yao haina uchangamfu wakilinganishwa na wale wa umri mdogo.

“Napendelea mili ya wanawake wachanga. Mwili wa mwanamke wa miaka 25 ni wa ajabu, mwili wa mwanamke wa miaka 50 hauna ajabu yoyote,” akasema.

Matamshi hayo yamevutia hisia kali, huku watu wakimkashifu kote mitandaoni.

Bi Marina Fois ambaye ni mwigizaji alirejelea matamshi hayo kwa njia ya kejeli akisema kwa kuwa anaelekea kufikisha miaka 49 amesalia na “mwaka mmoja na siku 14” ‘kulala’ na mwandishi huyo.

Watumizi zaidi wa mitandao ya kijamii walizidi kumkashifu mwandishi huyo, ambaye ana miaka 50, wakiyaona matamshi yake kama ya dharau dhidi ya watu wa umri huo.

Mwandishi mmoja wa habari alichapisha picha ya sehemu ya makalio yake na kuandika “makalio ya mwanamke wa miaka 52, hujui unachokikosa wewe.”

Wengine walizidi kutuma picha za watu mashuhuri ambao wanafahamika ulimwenguni na ambao licha ya kuwa na umri huo, bado wana mwonekano wa kuvutia.

Bw Moix ni mtangazaji, mwelekezi na mwandishi aliyeshinda tuzo ambaye anafahamika kwa kutoa matamshi ambayo wakati mwingi huibua hisia kali.

Katika gazeti hilo, matamshi mengine aliyotoa ambayo yalikashifiwa ni kuwa yeye hupendelea kujihusisha na wanawake kutoka Korea, China na Japan haswa.

Mambo yalipozidi na kashfa kumsonga, alieleza kituo kimoja cha redio kuwa hawezi kulaumiwa kutokana na ‘ladha yake’ ya wanawake. “Napenda yule napenda na siwezi kushtakiwa kwa ajili ya ladha yangu.”