Kimataifa

Netanyahu: Tutalipiza kisasi Iran, lakini baadaye kidogo

Na MASHIRIKA October 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

JERUSALEM, ISRAEL

ISRAEL imesema kuwa itatilia manani maoni ya Amerika lakini mwishowe italipiza kisasi dhidi ya Iran iliyowavamia mapema mwezi huu.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema hawajasahau kitendo cha Oktoba 1 ambapo Iran ilirusha roketi 200 nchini humo.

Iran ilifanya hivyo kulipiza kisasi kufuatia mauaji ya Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah na Kamanda wa Majeshi ya Kiislamu wa Iran Abbas Nilforoushan pamoja na kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh mapema mwaka huu.

“Tutasikiliza Amerika lakini tutafanya uamuzi wa mwisho ambao utazingatia maslahi ya raia wa Amerika,” akasema Netanyahu hapo Jumanne.

Kauli yake inafuatia ripoti kuwa Amerika imeiambia Israel ivamie makambi ya majeshi ya Iran lakini si vituo vya kutengeneza silaha hatari za kinuklia au zile za kawi.

Amerika inahofia Israel ikivamia vituo vya uundaji wa kinuklia, basi vita vikali huenda vikazuka ulimwenguni na Amerika itahusishwa.

Wiki jana kulikuwa na mazungumzo kati ya Waziri wa Ulinzi wa Amerika Lloyd Austin na mwenzake wa Israel Yoay Gallant ambapo wawili hao walikubali kuwa kwa sasa Israel haitalipiza kisasi úchokozi’ wa Iran kwa sasa.

Gallant alikuwa ameahidi kuwa Israel italipiza kisasi na Iran ijiandae kwa maangamizi makali ambayo haitawahi kusahau.

Kwa zaidi ya mwaka moja ambao kumekuwa na vita Gaza, Israel imezidisha vita kwenye mpaka wake na Palestina huku zaidi ya watu 42,000 wakiuawa.

Pia Israel imekuwa ikipambana na wanamgambo wa Hezbollah kule Lebanon, vita ambavyo vimezua uhasama mkubwa kati yake na Iran.