Kimataifa

Nkurunziza kupata donge nono akistaafu kuanzia Mei

January 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

GITEGA, BURUNDI

BUNGE la Burundi limepitisha sheria inayotoa idhini kwa serikali ya nchi hiyo kumlipa Rais Pierre Nkurunziza Sh53 milioni (dola za Amerika 530,000) atakapoondoka afisini.

Rais huyo ameahidi kutowania urais kwa mara nyingine katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Mei 2020.

Mnamo  Juni 7, 2018, Nkurunziza akiwa jijini Gitega alitia saini uidhinishaji wa Katiba Mpya iliyopitishwa kupitia kura ya maamuzi iliyofanyika Mei 17, 2018, na ambayo ingemruhusu kuwania urais mwaka huu 2020 na kuhudumu kwa kipindi cha miaka saba.

Sasa yumkini alibadilisha wazo.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, Nkurunziza pia atakuwa akipokea mshahara hadi afe, nyumba ya kifahari na manufaa yote ambayo Makamu wa Rais hupata.

Wabunge pia walipendekeza kuwa Rais huyo apandishwe hadhi na aitwe Kiongozi Mkuu (Supreme leader) na Shujaa wa uzalendo (Champion of patriotism).

Kama kiongozi mkuu Nkurunziza bado anatarajiwa kuwa na mamlaka, hasa katika chama tawala, ambacho kinapigiwa upatu kushinda katika uchaguzi ujao.

Wananchi wametoa hisia mseto kuhusu hatua ya malipo ambayo Rais huyo atapokea baada ya kustaafu.

Wengine walikosoa hatua hiyo ya bunge ikizingatiwa kuwa taifa hilo ni mojawapo ya mataifa maskini duniani.

Lakini wengine walisema kuwa manufaa hayo yanafaa kama asante kwa Nkurunziza ambaye ametumikia taifa hilo katika cheo hicho cha juu.