Nyuklia: Afrika Kusini yajificha kwa mbawa za Urusi na Iran baada ya kukosana na Amerika
CAPE TOWN, AFRIKA KUSINI
AFRIKA Kusini imesema kuwa sasa itaegemea Urusi au Iran kupanua kiwanda chake cha kutengeneza nyuklia ya kuzalisha umeme, hatua ambayo huenda ikazorotesha zaidi uhusiano kati yake na Amerika.
Mbali na kutatiza uhusiano na Amerika, hatua hiyo pia itakwamisha mkataba uliotiwa saini na nchi hizo mbili kuimarisha sekta ya kawi Afrika Kusini.
Afrika Kusini ndilo taifa pekee barani Afrika ambalo lina kiwanda cha nyuklia ya umeme, Koeberg na inapanga kuongeza megawati 2,500 kumaliza tatizo la ukosefu wa umeme.
Tatizo hilo limekuwa likiathiri uchumi wa Afrika Kusini na pia kawi safi inalenga kupunguza uchafuzi wa mazingira.
“Hatuwezi kuwa na kandarasi ambayo inasema Iran au Urusi haziwezi kutuma maombi ya kupata mkataba wa kustawisha kiwanda chetu cha nyuklia,” akasema Waziri wa Madini na Petroli, Gwede Mantashe.
Waziri huyo ni kati ya maafisa wa serikali ambao wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Afrika Kusini inapanua kiwanda chake cha nyuklia.
“Kama wao ndio bora na ofa yao inaturidhisha, basi tutawapa kazi hiyo,” akaongeza.
Afrika Kusini imekuwa kwenye mizani na kumulikwa na Amerika baada ya utawala wa Rais Donald Trump kutoa amri ya kusitisha msaada wowote wa kifedha kwa nchi hiyo.
Kati ya yaliyosababisha amri hiyo itolewe, ni madai kuwa Afrika Kusini imeimarisha uhusiano wake na Iran kustawisha kiwanda chake cha kinyuklia kwa ajili ya kibiashara na kuwa na uwezo mkubwa wa kijeshi.
Hata hivyo, Rais Cyril Ramaphosa aliweka wazi kuwa Afrika Kusini haina makubaliano yoyote na Iran katika uundaji na ustawishaji wa kiwanda chake cha kinyuklia.
Zabuni ya miradi ya nyuklia ambayo Afrika Kusini ilitarajiwa kutoa mwaka jana, imechelewa kutokana na vikwazo vya kisheria.
Vikwazo hivyo vilitokana na kesi iliyowasilishwa na chama cha upinzani DA ambayo kwa sasa ni sehemu ya serikali ya muungano.
Amerika na Afrika Kusini zimekuwa zikiendeleza mazungumzo kwa zaidi ya miaka 10 kuhusu mkataba wa nyuklia ambapo Amerika ingeuzia nchi hiyo mafuta na vifaa mbalimbali.
Hata hivyo, idara ya kawi haikufafanua iwapo amri ya Rais Trump itaathiri mazungumzo kati ya Amerika na Afrika kuhusu sekta ya kawi.
Awali Amerika na Afrika Kusini zilikuwa na mkataba kuhusu kuimarisha sekta zao za kawi kati ya 1997 hadi Disemba 2022 lakini haikurefushwa.
Mazungumzo kuhusu mkataba mpya yalikuwa yamekamilishwa lakini pande zote hazikuwa zimetia saini.
Kukosa kurefushwa kwa mkataba huo kutaathiri Afrika Kusini ambayo kiwanda chake cha umeme, Eskom, kimekuwa kikitegemea mafuta ya Amerika.
Kando na kawi, Rais Trump alisitisha msaada kwa Afrika Kusini ikidai kuwa sera zake zinawabagua watu weupe na kuwanufaisha wale weusi.