Kimataifa

Ombaomba akamatwa kwa kubaka mama msamaria mwema

January 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAUME aliyejifanya hana pa kuishi nchini Uingereza na kuishi maisha ya kuombaomba alikamatwa na polisi, baada ya kumbaka mama aliyejaribu kumsaidia.

James Campbell, mwanamume wa miaka 31 anadaiwa kumfuata mwanamke huyo wa miaka 57 hadi kando ya barabara, wakati mwanamke huyo alimwona bila jaketi na kutaka kujua ikiwa alikuwa sawa.

Campbell alipomfikia anadaiwa kumtaka mama huyo kumpa busu kwa lazima, kisha akambaka. Hii ilikuwa licha ya mwanamke huyo kumbembeleza asifanye hivyo, lakini mshukiwa akamtaka kukimya.

Mahakama Kuu ya Glasgow ilielezwa kuwa Campbell amekuwa akiombaomba katika barabara ya Buchanan, jijini Glasgow akiwa amevalia shati ya kandanda na kujifunika kwa bendera, licha ya kuishi na mamake eneo la Paisley.

“Inaeleweka kuwa alikuwa akipata kati ya Sh4000 na Sh10,000 kila siku kutokana na kuombaomba,” kiongozi wa mashtaka akaeleza korti.

Kisa chenyewe kilitendeka mnamo Agosti 16, mwaka uliopita, wakati mwanamke mdhulumiwa alimwona akiombaomba saa kumi na mbili jioni.

Mwanamke huyo alidaiwa kutaka kujua ikiwa alikuwa sawa kwani mvua ilikuwa ikinyesha, na wakazungumza kwa takriban dakika kumi.

Lakini jamaa huyo anadaiwa kumfuata na akakataa kurudi alikokuwa, akimtaka mama huyo kumpa busu, kabla ya kumvamia.

“Alimweleza mwanamke huyo, ‘ninakupenda, ninataka uwe mpenzi wangu’, naye akamjibu ‘wacha usumbufu, hata sikujui,” kiongozi wa mashtaka Angela Gray akaeleza korti.

Korti ilizidi kuelezwa kuwa mwanamke huyo alipambana na Campbell kwa muda akimbembeleza asimtendee unyama huo, japo mshukiwa hangesikia kitu.

Ni mpita njia aliyeona kisa hicho kikiendelea na kuwapigia polisi simu. Walipofika walimpata Campbell akimbaka mama huyo na wakamwondoa kwa nguvu. Alikuwa amjeruhi katika sehemu za mapaja.

Alipokamatwa, mshukiwa anadaiwa kuwaambia polisi “alihitaji ngono ya fujo, basi nikampa.”

Kisa hicho cha aibu kilinakiliwa na kamera za CCTV.

Jamaa huyo amekuwa akizuiliwa na polisi tangu wakati huo. Aidha, ana historia ya vifungo vingine mbeleni.

Atasomewa hukumu na korti mnamo Machi 1.