Kimataifa

Paa za majengo ya ubalozi wa Kenya ughaibuni zimetoboka – Ripoti

August 30th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

MASHIRIKA na PETER MBURU

OFISI za idara za ubalozi za Kenya katika mataifa tisa ziko kwenye hali ya kustaajabisha, huku zingine zikiwa na paa zilizotoboka na mabalozi kutumia magari ya hadhi ya chini kufanya shughuli za kidiplomasia.

Kulingana na ripoti iliyofikishwa bungeni na mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi na Uhusiano wa Nje Katoo Ole Metito Jumatano, taswira inayojengeka ni ile ya ubalozi ulioishiwa na ambao hauwezi kununua vifaa vya msingi.

Ubalozi wa Kenya Washington DC, Marekani kwa mfano una madirisha ya mbao ambayo yamechina kutokana na hali ya uzee na kusalia kwa miaka mingi bila kurekebishwa, inasema ripoti hiyo.

“Paa yake ya mabati na ujenzi ulioiimarisha aidha zilikuwa zimeharibika vibaya na kulikuwa na kutobokatoboka. Mifereji aidha ilikuwa imeharibika vibaya,” ripoti ya kamati hiyo ikazidi kusema.

“Paa nyingi za ndani zinaonyesha kuwa ziliwahi kuadhiriwa mbeleni na kuharibika, kutokana na kutoboka kwa paa ya juu ama mabati,” ripoti hiyo ikazidi kusema.

Kamati hiyo ilisema jumba hilo limekuwa likizidi kuharibika kadri muda unavyosonga, ikisema likilinganishwa na majumba yaliyokaribiana, ni wazi kuwa imetelekezwa.

Aidha, kamati hiyo ilisema wengi wa wakenya wanaofanya kazi katika mashirika ya ubalozi Korea Kusini, Beijing- Uchina na Tokyo- Japani waliondolewa na hawajarejeshwa hadi sasa, jambo ambalo limesababisha kukosekana kwa wafanyakazi.

Ilisema katika balozi za Uchina na Japani kuna nafasi kubwa ambazo zinaweza kujengwa nyumba za makao ya wafanyakazi.

Katika ubalozi wa Vienna, Australia ukosefu wa pesa umewafanya maafisa wa ubalozi huo kukosa kutembea katika miji mingine yoyote mbali na Jiji Kuu la nchi hiyo, na pia ubalozi umekosa pesa za kuandaa maonyesho ya kuuza bidhaa za Kenya huko.

Ripoti hiyo iliendelea kutoboa kuwa wafanyakazi katika ubalozi wa Kenya kwenye umoja wa mataifa (UN) wamekuwa wakicheleweshewa mishahara, huku ukiwa na madeni mengine kutokana na wizara ya fedha kuchelewa kuutumia pesa kwa wakati unaofaa.

Kamati hiyo ilitembelea majengo ya balozi hizo kati ya Aprili 19 na Juni 22, 2018 kwa nia ya kukagua hali yake katika mataifa ya Korea, Uchina, Japani, Uswizi, Australia, Urusi, Marekani na Canada.