Kimataifa

Papa Francis aitisha mazungumzo maaskofu wakiendelea kuwindwa

January 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MASHIRIKA

NICARAGUA

TAKRIBAN maaskofu 14 wametiwa mbaroni, kufuatia msako mkali dhidi ya Kanisa Katoliki nchini Nicaragua hatua ambayo imemsukuma Papa Francis kutoa wito wa kufanya mazungumzo.

Kwa mujibu wa orodha iliyoandaliwa na Martha Molina, mtaalamu wa masuala ya kanisa Nicaragua, ambaye anaishi nchini Amerika, Askofu Gustavo Sandino kutoka eneo la kaskazini la Jinotega, alikamatwa usiku wa mkesha wa Mwaka Mpya.

Sandino, alikamatwa Desemba 31, 2023 baada ya Misa ya Jumapili aliyoadhimisha huko Santa María de Pastasma katika Dayosisi ya Jinotega, Nicaragua.

Takriban mapadre 14 wamekamatwa katika siku za hivi karibuni, pamoja na waseminari wawili, Alester Saenz na Tony Palacio, na Askofu Isidoro del Carmen Mora Ortega wa Siuna.

Kuzuiliwa kwake ni tukio la hivi karibuni katika wimbi la kamatakamata ya Rais Daniel Ortega, ambayo ilianza Desemba 20.

Hata hivyo, hatua ya serikali ya kuwakamata viongozi hao wa kidini imepingwa vikali na wanaharakati mbalimbali.

Katika ibada ya Mwaka Mpya mjini Roma, Papa Francis alisema anafuatilia kwa karibu hali ilivyo nchini humo.

Uhusiano kati ya Kanisa na serikali ya Ortega ulidorora wakati wa maandamano ya kupinga mageuzi ya hifadhi ya jamii mwaka 2018, ambayo Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa yalisababisha vifo vya takriban watu 300.

Ortega alishutumu jumuiya ya kidini kwa kuunga mkono upinzani wakati wa maandamano, baada ya kanisa kuwakinga waandamanaji.

Kulingana na wanaharakati, watu walianza maandamano hayo kupinga ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu.

Hata hivyo, wasimamizi wa serikali na polisi hawajatoa maoni yao kuhusu kamatakamata hizo.

Ortega ni kiongozi wa zamani wa wapiganaji wa msituni ambaye alisaidia kuongoza mapinduzi ambayo yalipindua utawala uliokuwa ukiungwa mkono na Amerika mwaka 1979. Kisha alitawala nchi hiyo kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Alirejea madarakani mwaka wa 2007, na amekuwa akishutumiwa kwa ubabe huku akiwafukuza na kuwafunga wapinzani.

Mashirika kadhaa ya watu wa Nicaragua walio uhamishoni siku ya Jumapili walitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kujitenga na kuacha kuisaidia nchi hiyo hadi wapinzani 120 waliowekwa jela waachiliwe.

Haya yanajiri wakati ambapo kauli ya Papa Francis kuhusu ushoga ikiendelea kupingwa ulimwenguni.

Mnamo Desemba 19, 2023, Kiongozi wa Kanisa la Katoliki Papa Francis aliridhia mapadri kubariki wapenzi wa jinsia moja, katika mabadiliko ya sera yanayonuiwa kulifanya Kanisa kuwashirikisha wote ila bado ndoa za jinsia moja ni marufuku.