Kimataifa

Papa Francis aliagiza alikotaka azikwe kwenye wosia wake wa kiroho

Na BENSON MATHEKA April 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

PAPA Francis aliyefariki dunia Aprili 21 baada ya kuugua kiharusi aliagiza azikwe katika kanisa la Basilica of Saint Mary Major, Roma mahali ambapo daima alikimbilia kuomba kabla na baada ya kila safari yake ya kitume.

Agizo hilo limefichuliwa katika agano lake la kiroho ( wosia wa kiroho) lililoandikwa  Juni 29 2022, na kuchapishwa rasmi baada ya kifo chake kilichotokea Aprili 21, 2025.

Katika waraka huo wa kipekee, Papa Francis alieleza kwa unyenyekevu jinsi alivyotaka safari yake ya mwisho duniani imalizikie mahali hapo patakatifu pa Bikira Maria – Mama wa Yesu – ambaye alimkabidhi maisha yake yote ya huduma ya upadri na upapa.

“Ninapohisi machweo yanayokaribia ya maisha yangu ya duniani,natamani kuweka wazi matakwa yangu ya mwisho, yakihusiana tu na mahali pa mazishi yangu,” aliandika Papa Francis.

Alisisitiza kuwa mabaki yake yapumzishwe chini ya ardhi, katika kaburi lisilo na mapambo,  katikati ya Kanisa la Pauline na Kanisa la Sforza, ndani ya eneo hilo la kihistoria. Jina pekee litakaloandikwa kwenye kaburi lake ni:
Francis, aliagiza.

Katika agano hilo, Papa Francis alieleza kuwa gharama zote za mazishi zitagharamiwa na mfadhili, ambaye alikuwa ameandaa fedha hizo zitumwe Basilica of Saint Mary Major. Alitoa maagizo rasmi kwa Kadinali Rolandas Makrickas, Kamishna Maalum wa Basilica of Saint Mary Major, kuhakikisha maandalizi yatafuata agizo lake la kiroho.

Katika hitimisho la waraka huo, Papa aliandika maneno yenye mguso mkubwa wa kiroho na matumaini:

“Mateso yaliyoashiria sehemu ya mwisho ya maisha yangu namtolea Bwana, kwa ajili ya amani duniani na udugu kati ya mataifa.”

Papa Francis, anayekumbukwa kwa unyenyekevu wake, upendo kwa maskini, na msimamo wake thabiti kwa haki za binadamu, alitambua umuhimu wa kumaliza maisha yake duniani kwa ishara ya ibada ya kutafakari na imani thabiti.

Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika kuhudhuriwa na maelfu ya waumini na viongozi kutoka duniani kote.