Kimataifa

Papa Francis awataka Waamerika Wakatoliki kuchagua “shetani mzuri” kati ya Trump na Harris

Na MASHIRIKA na CHARLES WASONGA September 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

PAPA Francis amesema kuwa wagombeaji wawili wakuu wa urais nchini Amerika “hawathamini maisha” na kuwashauri wapiga kura Wakatoliki kuchagua “asiye mbaya zaidi” katika uchaguzi wa Novemba 5, mwaka huu, 2024.

Huku akirejelea sera ya mgombeaji wa chama cha Republican Donald Trump, Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani alisema ni makosa makubwa kwa kiongozi huyo kuwakataa wahamiaji.

Kwa upande mwingine, Papa Francis alitaja msimamo wa mgombeaji wa Democrat Kamala Harris wa kuruhusu uavyaji mimba kama “mauaji”.

“Wote wawili wanaenda kinyume na haki ya kuishi; awe yule anayewafurusha wahamiaji au yule anayewaua watoto wachanga,” Papa Francis aliwaambia wanahabari Jumamosi, Septemba 14, 2024 akikamilisha ziara yake ya siku 12 kusini mashariki mwa Asia.

Hata hivyo, Papa Francis alichelea kurejelea Harris na Trump kwa majina yao katika kauli zake.

Aliwahimiza Waamerika ambao ni waumini wa dini ya Katoliki kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi huo.

Hata hivyo, alifafanua kuwa yeye sio Mwamerika na hivyo hatashiriki katika upiga kura huo.

“Sio vizuri kususia kura. Sharti mtu apige kura. Lakini sharti mchague yule asiye mbaya zaidi. Asiye mbaya zaidi. Yule mwanadada au yule mwanamume? Sijui. Kila mtu atafakari kabla ya kupiga kura.”

Papa huyo mara kadhaa amelaani uavyaji mimba ambao ni kinyume na mafunzo ya Kanisa Katoliki.

“Kulazimisha mtoto kutoka kwa tumbo la mama ni mauaji kwa sababu huyu ni kiumbe mwenye uhai,” Francis akasema.

Kuhusu ahadi ya Trump ya kufurusha wahamiaji walioko Amerika, alisema hivi: “Kuwafurusha wahamiaji, kuwanyima nafasi ya kujiendeleza na kuwakosesha maisha sio jambo zuri,” akaeleza.

Mara kadha Trump ameahidi kufurusha wahamiaji haramu walioko Amerika endapo atashinda katika uchaguzi huo.

Kwa upande wake Kamala Harris, ameahidi kupanua upatikanaji wa huduma za uavyaji mimba nchini Amerika.

Papa Francis alitoa kauli yake siku chache baada ya Trump na Harris kushiriki katika mdahalo wa kwanza wa urais.

Wawili hao walitarajiwa kukabiliana tena kwenye jukwaa kama hilo kabla ya siku ya uchaguzi.

Hata hivyo, Trump ambaye ni rais wa zamani wa Amerika amesema hatashiriki mdahalo mwingine na Harris ambaye wakati huu anahudumu kama Makamu wa Rais wa Amerika.

Bw Joe Biden ndiye Rais wa sasa Amerika, na alimwachia Bi Harris kutoana kijasho na Trump.