Kimataifa

Papa Leo asikitikia mahangaiko ya Wapalestina katika misa ya Krismasi

Na BENSON MATHEKA, REUTERS December 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Leo, Alhamisi alisikitikia hali wanayopitia Wapalestina huko Gaza katika mahubiri yake ya Krismasi , akitoa wito wa moja kwa moja usio wa kawaida wakati wa ibada ambayo kwa kawaida siku ambayo Wakristo duniani kote huadhimisha kuzaliwa kwa Yesu.

Leo, ambaye ni papa wa kwanza kutoka Amerika, alisema simulizi la Yesu kuzaliwa zizini linaonyesha kuwa Mungu “alipiga hema” miongoni mwa watu dhaifu duniani.

Leo, ambaye aliadhimisha Krismasi yake ya kwanza tangu achaguliwe Mei kuchukua nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha Papa Francis, ana mtindo wa utulivu na wa kidiplomasia zaidi kuliko mtangulizi wake na kwa kawaida hujiepusha na masuala ya kisiasa katika mahubiri yake.

Hata hivyo, papa huyo mpya amekuwa akilalamikia mara kadhaa hali ya Wapalestina huko Gaza, na aliwaambia wanahabari mwezi uliopita kuwa suluhu pekee ya mzozo wa miongo kadhaa kati ya Israeli na Wapalestina lazima ihusishe kuundwa kwa taifa la Palestina.

Israel na Hamas walikubaliana kusitisha mapigano Oktoba baada ya miaka miwili ya mashambulizi makali ya mabomu na oparesheni za kijeshi, lakini mashirika ya misaada ya kibinadamu yanasema msaada bado unaingia kwa kiwango kidogo sana Gaza, ambako karibu wakazi wote hawana makazi.

Katika ibada ya Alhamisi iliyohudhuriwa na maelfu ya waumini katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Leo pia alilalamikia hali ya watu wasio na makazi duniani kote pamoja na uharibifu unaosababishwa na vita vinavyotikisa dunia.

“Miili ya watu wasio na ulinzi ni dhaifu, imejaribiwa na vita vingi, vinavyoendelea au vilivyomalizika, na kuacha nyuma vifusi na majeraha yasiyopona,” alisema papa.

“Dhaifu pia ni akili na maisha ya vijana wanaolazimishwa kubeba silaha, ambao wakiwa mstari wa mbele huhisi upuuzi wa yale wanayotakiwa kufanya na uongo unaojaza hotuba za majivuno za wale wanaowatuma kwenda kufa,” aliongeza.

Baadaye Alhamisi, papa anatarajiwa kutoa ujumbe na baraka zake za Urbi et Orbi (kwa mji na dunia), ambazo kwa kawaida hushughulikia migogoro ya kimataifa.