Kimataifa

Polisi mjamzito aua mwanamume kwa kumkejeli

August 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na ANDREW BAGALA na ANTHONY WESAKA

DEREVA wa jaji alipigwa risasi akafariki baada ya kumkejeli polisi mjamzito kwamba bunduki yake ilikuwa hafifu.

Duru zilisema polisi huyo, Daisy Nagasha, ambaye ni mlinzi wa jaji aliandika taarifa kuwa marehemu Ismail Mayiga alifika kazini mwendo wa saa moja asubuhi na kuanza kumwambia jinsi uume wake ulikuwa na uwezo wa ‘kufyatua risasi kali zaidi’ kuliko bunduki aliyobeba.

Katika taarifa yake, alieleza jinsi Mayiga alivyoanza kuchezea bunduki hiyo licha ya kuonywa akome.

“Nilishikilia bunduki yangu na kwa bahati mbaya risasi ikafyatuka na kumpiga tumboni,” alinukuliwa kuandika kwenye taarifa kwa Kituo cha Polisi cha Kabalagala.

Msemaji wa polisi, Emilian Kayima, alisema wanachukulia kisa hicho kama ajali.

 

“Ni kisa cha kuhuzunisha. Kwa sasa kila ishara inayonyesha kuwa haikuwa mauaji ya kusudi bali ni ajali. Lakini bado uchunguzi unaendelea,” akasema kwenye taarifa.

Polisi walisema watachunguza kama bunduki hiyo ina alama za vidole vya marehemu ili kuthibitisha kama madai ya Nagasha ni ya kweli.

Duru zilisema polisi wanaolinda watu mashuhuri kama vile majaji, huhitajika kuweka bunduki zao tayari kwa ufyatuaji endapo kutakuwa na tukio la dharura na hivyo basi kuna uwezekano wa risasi kufyatuka bunduki inapoguswa bila tahadhari.