Kimataifa

Polisi wamwagwa barabarani na mitaani na kufaulu kuzima maandamano Tanzania

Na REUTERS December 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

DAR ES SALAAM, TANZANIA

POLISI na wanajeshi Desemba 9, 2025 walimwagwa Dar es Salaam na maeneo mbalimbali kuwazuia wanaharakati na raia ambao walikusudia kushiriki maandamano.

Shughuli hiyo ilikuwa ya kuonyesha kero zaidi kuhusiana na uchaguzi wa mnamo Oktoba 29 ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alishinda kwa asilimia 98 ya kura na kuwafungia nje wapinzani wake wakuu.

Jumanne ilikuwa siku ya kuadhimisha uhuru wa Tanzania uliopatikana mnamo 1961 kutoka kwa Uingereza.

Hata hivyo, serikali ilizima sherehe kutokana na kuhofia ghasia na fujo kwenye maandamano hayo na kuwataka raia wakae nyumbani.

Utawala wa Rais Suluhu ulidai kuwa maandamano hayo yalikuwa yakitumika kuhujumu na kusambaratisha uongozi wake, akidai kuwa alishinda kura kwa njia halali.

Uchaguzi wa Urais na Ubunge mnamo Oktoba 29 ulisababisha ghasia na wimbi la fujo Tanzania, tukio ambalo halikuwa limetokea nchini humo tangu kupatikana kwa uhuru.

Umoja wa Mataifa (UN) unadai kuwa mamia ya watu waliuawa kwenye maandamano hayo.

Jumanne, usalama ulikuwa umeimarishwa katika maeneo mbalimbali huku watu wakisalia nyumbani katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Mwanza miongoni mwa miji mingine mikuu.

Jijini Dar es Salaam, polisi walikuwa kila mahali na kila aliyekuwa akitembea alisimamishwa na kitambulisho chake kuangaliwa huku akikaguliwa na kuulizwa maswali.

Hali ilikuwa tulivu Dar es Salaam lakini jiji hilo lilikuwa kama mahame. Mitandaoni, baadhi ya wanaharakati walidai kulikuwa na maandamano madogo yaliyokuwa yameanza katika baadhi ya maeneo ya jiji hilo.

Hata hivyo, shirika la Reuters halikuwa limethibitisha hilo. Msemaji wa polisi Tanzania pia hakujibu maswali kuhusu jinsi ambavyo hali ilivyokuwa katika maeneo mbalimbali na iwapo nchi iliathirika kiuchumi.

Rais Suluhu mwezi uliopita aliteua jopo la kuchunguza ghasia za baada ya uchaguzi ila mara si moja amekuwa akikanusha kwamba maafisa wa usalama walitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia.

Wanaharakati wa UN wiki jana walisema kuwa zaidi ya watu 700 waliuawa kwenye ghasia za baada ya uchaguzi.

Serikali ndiyo ilithibitisha kuwa watu walikufa lakini haijatoa takwimu zake kuhusu walioaga dunia kwenye uchaguzi huo.

Wiki jana, Amerika ilitangaza kwamba ilikuwa ikitathmini upya uhusiano wake na Tanzania kuhusiana na ripoti kuwa serikali ilikuwa ikiendeleza mauaji dhidi ya raia.

Pia Amerika ilikasirishwa na ukosefu wa uhuru wa kujieleza, kuabudu na pia ikadai Tanzania ilikuwa ikiiwekea vikwazo vya uwekezaji.

Miezi iliyoelekea uchaguzi mkuu, viongozi wa upinzani pamoja na makundi ya wanaharakati walishutumu serikali kuhusika na vitendo vya watu kupotea kupitia njia tatanishi.

Rais Samia mwaka jana alisema kuwa ameamrisha uchunguzi kuhusu utekaji nyara uliotokea lakini hakuna matokeo ambayo yametangazwa.