Kimataifa

Presha za Gen Z hatimaye zamtorosha Rais Rajoelina wa Madagascar

Na MASHIRIKA, CHARLES WASONGA October 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ANTANANARIVO, Madagascar

RAIS wa Madagascar Andry Rajoelina aligura taifa hilo Jumatatu, Oktoba 13, 2025 kutokana na presha zilizotokana na maandamano ya wiki kadhaa dhidi ya serikali yake.

Maandamano yaliyoanza Septemba 25, yaliongozwa na vijana waliochukizwa na utawala mbaya, kukithiri kwa ufisadi na kupanda kwa gharama ya maisha.

Rais Rajoelina alitoroshwa na ndege moja ya kijeshi ya Ufaransa kutokana na ombi kwa Rais Emmanuel Macron, kulingana na Radio France International.

Awali, ubalozi wa Ufaransa nchini Madagascar ulisema kuwa nchi hiyo haitatoa usaidizi wa kijeshi kwa taifa hilo ambalo lilikuwa chini ya utawala wake kabla ya kujipatia uhuru.

Mnamo Jumamosi, Rais Rajoelina alielezea hofu kuhusu njama ya wanajeshi kufanya mapinduzi dhidi ya serikali yake, baada ya baadhi yao kuwaunga mkono waandamanaji.

Aidha, kikosi maalum cha wanajeshi kwa jina, CAPSAT, kilitangaza kutwaa usimamizi wa Jeshi la Madagascar.

Kupitia taarifa kutoka Ikulu, Rais Rajoelina alisema: “Afisi ya Rais ingependa kujulisha taifa na jamii ya kimataifa kuna mipango ya kutwaliwa kwa mamlaka kinyume cha sheria na kwa nguvu kinyume cha Katiba na misingi ya kidemokrasia.”

Hata hivyo, Rais huyo aliwahakikishi raia kwamba angali nchini Madagascar na anasimamia shughuli za kitaifa.

Isitoshe, Rajoelina Jumatatu, Oktoba 13, 2025, alitarajiwa kutoa hotuba kwa taifa kuhusu hali nchini humo na hatua zilizowekwa kurejesha utulivu.

Awali, Jumamosi usiku, Waziri Mkuu mpya Ruphin Fortunat Zafisambo alitoa hakikisho kuwa serikali iko tayari kusikiza na kuzungumza na makundi yote- vijana, vyama vya wafanyakazi na jeshi.

Lakini mnamo Jumapili jioni, Jenerali Demosthene Pikulas kamanda wa kikosi cha Capsat, alitawazwa kuwa mkuu wa majeshi katika sherehe iliyofanyika katika makao makuu ya jeshi la Madagascar.

Sherehe hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Vikosi vya Ulinzi Manantsoa Deramasinjaka Rakotoarivelo.

“Nampa baraka zangu,” waziri huyo alisema akimrejelea Pikulas.

Akiongea na wanahabari baada ya sherehe hiyo, Pikulas alisema machafuko yaliyoshuhudiwa nchini Madagascar ndani ya wiki kadhaa zilizopita “hayakuwa yametarajiwa kutokea.”

“Kwa hivyo jeshi liko na wajibu wa kurejesha utulivu na amani maeneo yote nchini humu,” akaeleza.

Alipoulizwa ikiwa angetaka Rais Rajoelina ajiuzulu, Pikulas alikataa kuzungumzia “siasa ndani ya makao makuu ya kijeshi.”

Jumamosi, kikosi cha Capsat kilisema hakingewafyatulia risasi waandamanaji huku kikitoa wito kwa wanajeshi wengine “kuungana nasi” kushikilia msimamo huo.

Baadaye alasiri, wanachama wa kikosi hicho waliondoka katika kambi yao iliyoko kitongoji cha Soanierana, kusini mwa Antananarivo kwa magari ya kijeshi wakielekea uwanja wa May 13 Square. Waliandamana na maelfu ya waandamanaji waliokuwa wakiwashangilia.

Jenerali mmoja wa Capsat alisema Jumamosi kwamba mwanajeshi wao mmoja na mwanahabari waliuawa katika machafuko hayo.

Umoja wa Mataifa ulisema kuwa angalau watu 22 waliuawa mwanzoni mwa maandamano hayo mnamo Septemba 25.

Hata hivyo, Rais Rajoelina alipinga ripoti hiyo wiki jana akisema ni watu 12 pekee waliokuwa wakipora na kuharibu mali waliuawa.

Mwanzoni, maandamano nchini Madagascar yalishirikishwa na vijana wa Gen Zs, waliotiwa shime na maandamano yaliyoongozwa na kizazi kama hicho katika mataifa ya Indonesia na Nepal.

Mnamo Septemba 29, Rais Rajoelina aliwafuta kazi mawaziri wake ili kutuliza fujo. Hata hivyo, waandamanaji walisema hatua hiyo haitoshi huku wakishinikiza kujiuzulu kwa rais mwenyewe, uongozi wa bunge na majaji wote wa mahakama ya kikatiba.