Kimataifa

Putin adokeza yuko tayari kusitisha vita nchini Ukraine

May 25th, 2024 1 min read

NA MASHIRIKA

MOSCOW, URUSI

HATIMAYE Rais wa Urusi Vladimir Putin amedokeza kuwa yuko tayari kusitisha vita nchini Ukraine, chini ya makubaliano yanayolinda masilahi ya nchi yake, kulingana na duru za serikali ya Urusi.

Hata hivyo, kiongozi huyo alionya kuwa yuko tayari kuendelea na vita ikiwa Ukraine na mataifa ya Magharibi zisipokubali matakwa yake.

Duru za serikali ya Urusi ziliambia shirika la habari la Reuters kuwa Putin aliwaelezea baadhi ya washauri wake kuhusu msimamo wake mpya huku mataifa ya Magharibi yakijaribu kuvuruga mazungumzo.

Naye Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amefuata nyayo za nchi hizo na kukataa mazungumzo.

“Putin anaweza kuendelea kupigana kwa muda mrefu lakini Putin pia yuko tayari kwa makubaliano ya kukomesha vita,” akasema afisa mwingine mwenye cheo cha juu na ambaye amewahi kufanya kufanya kazi na Putin kwa muda mrefu.

Afisa huo, sawa na wengine, waliomba majina yao yabanwe kwa sababu suala hilo ni nyeti mno.

Akiongea Ijumaa wiki jana kwenye kikao na wanahabari jijini Belarus, Rais Putin alisema mazungumzo ya amani yanafaa kuanza upya.

“Mazungumzo yarejelewe,” akasema, akiongeza kuwa mazungumzo hayo yaendeshwe kwa misingi ya “hali halisi ilivyo sio kwa misingi ya kile upande mmoja unataka”.

Lakini Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Ukraine Dmytro Kuleba alisema, kupitia mtandao wa X, kwamba Putin anajaribu kuvuruga mkutano wa viongozi kuhusu amani utakaofanyika Uswizi mwezi ujao.

“Anafanya hivyo, kwa kuwatuma maafisa wake kueneza habari bandia kuhusu kujitolea kwake kusitisha vita,” Kuleba akaeleza.

“Tujuavyo ni kwamba Putin hana nia ya kusitisha mashambulio dhidi ya Ukraine. Ni nguvu na sauti za pamoja za mataifa ya ulimwengu zinazoweza kumlazimisha kukumbatia amani badala ya vita,” Waziri huyo akaongeza.

Naye Mykhailo Podolyak, ambaye ni mmoja wa washauri wa Rais wa Ukraine, alisema Putin anataka nchi za Magharibi zikubali kuwa amezishinda.