Kimataifa

Qatar yaondolea Wakenya baadhi ya vikwazo vya usafiri

October 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Mamia ya wahamiaji kutoka Kenya wanaoishi Qatar na kufanya kazi kama vijakazi, wanadhifishaji au maderava wana uhuru wa kurejea nyumbani bila kuzuiliwa.

Hii ni  baada ya Qatar kuondoa visa ya kuondoka nchini humo, ambayo uhitaji wafanyikazi kutafuta idhini kutoka kwa waajiri wao kabla ya kuondoka nchini humo.

Kulingana na Qatar, sheria hiyo mpya itaanza kutekelezwa kuanzia wiki hii.

Serikali ya Kenya ilikaribisha hatua hiyo kwa kusema inaibua matumaini ya kukomeshwa kwa dhuluma dhidi ya wafanyikazi wasio raia wa Qatar.

Serikali sasa inataka mataifa mengine ya Mashariki ya Kati kuiga Qatar na kuondoa vikwazo vya kufanya kazi nchini humo.

Mataifa ya Mashariki ya Kati mara nyingi yameshutumiwa kwa kudhulumu wafanyikazi kutoka mataifa mengine hasa kutokana na mfumo mbaya na uliopitwa na wakati wa sheria.

Wakenya wengi, hasa vijakazi wamerejea nchini na kulalamika kuteswa na waajiri wao katika mataifa ya Mashariki ya Kati.

Licha ya mateso hayo, idadi kubwa ya Wakenya huzuru Mashariki ya Kati kwa kazi, hasa kupitia kwa mawakala.