Kimataifa

Rais Barrow asema Gambia inakaribia kupata maridhiano

September 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na AFP

RAIS wa Gambia, Adama Barrow, alisema Alhamisi kwamba nchi hiyo inaelekea kupata maridhiano, miaka miwili na nusu baada ya mtangulizi wake Yahya Jammeh kwenda uhamishoni akikabiliwa na madai ya kutesa raia.

Jammeh, aliyetawala nchi hiyo kwa miaka 22, alitoroka Januari 2017 baada ya kushindwa uchaguzini ingawa mwanzoni alidinda kuondoka mamlakani.

Tume ya Ukweli na Maridhiano imekuwa ikipokea ushahidi wa ukatili kutoka kwa watu wakiwemo waliokuwa wakitumiwa na Jammeh kuua watu.

Tangu Januari, waathiriwa wamekuwa wakiandamana nje ya ofisi za tume.

“Kupitia tume hii, waathiriwa na waliofiwa wanafahamu ukweli na waliotekeleza mauaji wanapatana na familia za waathiriwa na wao binafsi,” Barrow alisema kwenye taarifa bungeni.

Wiki jana, serikali ya Gambia ilisema kwamba inanuia kumshtaki Jammeh kwa madai ya wizi na ufisadi.

Rais huyo wa zamani alipata vipande zaidi ya 280 vya ardhi, visiwa, misitu na mbuga za wanyama alipokuwa mamlakani, kulingana na Waziri wa Haki, Abubacarr Tambadou.