• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Rais Ruto na Waziri Blinken wafanya mazungumzo kuhusu Haiti

Rais Ruto na Waziri Blinken wafanya mazungumzo kuhusu Haiti

NA CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Masuala ya Kigeni wa Amerika Antony Blinken Jumamosi, Machi 9, 2024 alifanya mazungumzo na Rais William Ruto kuhusu mzozo wa Haiti.

Wawili hao walikariri kujitolea kwa nchi zao kufanikisha kibarua cha kikosi cha pamoja cha kuleta amani katika taifa hilo (MNSM), kulingana na taarifa kutoka kwa Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika.

“Waziri Blinken na Rais wa Kenya William walielezea kujitolea kwa mpango wa kutumwa kwa Kikosi cha Walinda Usalama kutoka Mataifa Mbalimbali Kulinda Usalama Haiti (MNSSM),” ikasema taarifa hiyo bila kutoa maelezo zaidi kuhusu mazungumzo kati ya wawili hao.

Haiti ilitumbukia katika hali hatari Jumapili iliyopita baada ya mapigano kuzuka wakati ambapo Waziri Mkuu Ariel Henry alikuwa jijini Nairobi kutia saini mkataba wa usalama kuiwezesha Kenya kutuma maafisa wake wa polisi kudumisha amani Haiti.

Mnamo Oktoba, mwaka jana (2023) Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) liliipa Kenya kibali cha kuongoza kikosi cha walinda usalama kutoka nchi mbalimbali kuleta amani katika taifa la Haiti ambalo limezongwa na mapigano yanayoendeshwa na magenge ya wahalifu.

Japo Kenya ilikubali kuongoza mchakato huo wa kuleta amani Haiti, Mahakama Kuu ilitaja hatua hiyo kama haramu kwa misingi kuwa Kenya haina mkataba wa kiusalama na taifa hilo la eneo la Caribbean.

Hii ni baada ya kiongozi wa Chama cha Thirdway Alliance Dkt Ekuru Aukot kuwasilisha kesi kupinga mpango huo ambao umeidhinishwa na baraza la mawaziri pamoja na bunge la kitaifa.

Ghasia zilizozuka Haiti baada ya ziara ya Waziri Mkuu Henry nchini zilichangia kuachiliwa huru kwa zaidi ya wafungwa 4,000 na kufungwa kwa uwanja wa kimataifa wa ndege nchini humo, kufungwa kwa shule na kusitishwa kwa utoaji huduma katika afisi za serikali.

Hali hiyo ilimlazimu Henry kukwepa kurejea nchini humo baada ya ziara yake Kenya na badala yake kutua katika nchi jirani ya Jamhuri ya Dominican anakopewa hifadhi.

Haiti imekuwa ikishuhudia machafuko baada ya Rais wake Jovenel Moïse, kuuawa Julai 2021.

 

  • Tags

You can share this post!

Mwaura alaani mauaji ya mwanablogu 

Al Shabaab wajeruhi askari 9 

T L