Kimataifa

Rais wa Ethiopia atimuliwa baada ya kukosana na Waziri Mkuu Abiy Ahmed

Na CHARLES WASONGA NA MASHIRIKA October 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

BUNGE la Ethiopia limeidhinisha uteuzi wa rais mpya kuchukua mahala pa rais wa kwanza wa kike nchini humo Sahle-Work Zewde.

Duru zinasema kuwa  rais huyo alitimuliwa baada ya kukosana na Waziri Mkuu Abiy Ahmed.

Taye Astike Selassie, ambaye amekuwa akihudumu kama Waziri wa Masuala ya Kigeni, ameteuliwa kuwa rais mpya wa Ethiopia, wadhifa ambao hauna mamlaka makuu.

Nchini Ethiopia, afisi ya Waziri Mkuu ndio yenye mamlaka makuu kisiasa na kiserikali.

Hatua ya Waziri huyo mkuu kuunga mkono kuteuliwa kwa Sahle-Work kuwa rais, ilitajwa kama ushindi mkubwa katika kufikiwa kwa usawa wa kijinsia katika siasa za Ethiopia.

Mnamo Jumamosi Sahle-Work aliweka ujumbe mfupi na wenye maana fiche katika mtandao wa X, akiashiria kuwa hakuwa na furaha na ndio maana amenyamaza kwa muda wa mwaka mmoja uliopita.

Rais wa kwanza wa kike Ethiopia Sahle-Work Zewde (kushoto) alipokuwa na uhusiano mzuri na Waziri Mkuu Abiy Ahmend. Picha|Maktaba

Duru zilisema kuwa kiongozi huo alikuwa akisubiri muhula wake ukamilike mwezi huu ili ajiondoe kutoka wadhifa huo.

Wakati wa hatamu yake kama rais wa Ethiopia, Sahle-Work alitumia muda mwingi kuhimiza amani nchini humo.

Hata hivyo, alikosolewa wakati mwingi kwa kukosa kulaani dhuluma za kijinsia zilizoshuhudiwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe katika eneo la Tigray.

Lakini inaaminika kuwa amekemea zaidi mapigano yanayoendelea sasa katika maeneo ya Oromia na Amhara.

Katika eneo la Amhara, wanajeshi wa Ethiopia wamekuwa wakipambana na kundi moja la wapiganaji eneo hilo. Mapigano hayo yamechangia kuuawa kwa watu wengi na maafisa wa usalama kuelekezewa tuhuma za kutekeleza uhalifu wa kibinadamu.

Rais Taye, mwenye umri wa miaka 68 ni mwanadiplomasia mwenye tajriba kubwa kwani amewahi kuhudumu katika Umoja wa Mataifa na Misri.

Aliapishwa rasmi mbele ya Wabunge mnamo Jumatatu.

Kuondolewa kwa Sahle-Work kunamaanisha kuwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ndiye amesalia rais wa kipekee wa kike barani Afrika.