Rais wa Marekani aliyedaiwa mabilioni akiwa madarakani
Na MASHIRIKA
WASHINGTON, AMERIKA
RAIS wa zamani Bill Clinton, amefichua kwamba alikuwa na madeni ya dola milioni 16 (Sh1.6 bilioni) alipokamilisha hatamu yake ya uongozi mwaka wa 2001.
Akifanyiwa mahojiano kwenye runinga ya NBC, Clinton alifichua kwamba alipokuwa uongozini alikumbwa na matumizi mengi ya fedha kwenye kesi zilizomhusisha na kashfa mbalimbali.
Miongoni mwa kashfa zilizomkumba ni kuhusu uhusiano wake wa kimapenzi na Monica Lewinsky ambaye alikuwa akifanya kazi afisini mwake, uamuzi wa bunge kumng’atua mamlakani na uamuzi wa Jimbo la Arkansas kufutilia mbali leseni yake ya uwakili.
Kulingana na mashirika ya habari, alikuwa akipokea mshahara wa dola 200,000 (Sh20 milioni) na kiwango hicho hakingetosha kugharamia mawakili wake.
Hata hivyo, imesemekana matatizo haya ya kifedha hayakudumu kwa muda mrefu kwani alipata kazi za kufanya alipoondoka mamlakani.
Miongoni mwa kazi ambazo zilimtatulia hasara zake za kifedha ni kutoa hotuba na kuandika vitabu.
Zaidi ya hayo, mke wake Hillary pia alisaidia kuondoa madeni hayo kupitia kwa kazi zake za kisiasa na uandishi wa vitabu.
-Imekusanywa na Valentine Obara