Kimataifa

Ruto aahidi kuimarisha uchumi wa Afrika Mashariki anapochukua usukani kama mkuu wa EAC

Na CHARLES WASONGA December 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto sasa ndiye mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baada ya muhula wa mwaka mmoja wa Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kumalizika.

Atahudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja, kulingana na kanuni za EAC kuhusu uenyekiti.

Akiongea Jumamosi katika mkutano wa 24 wa Marais wa Mataifa wanachama wa EAC, Rais Ruto alipongeza uongozi wa mtangulizi wake akiutaja kama “wenye kuigwa” kwani umesheheni “maono”.

“Chini ya uongozi wake, jumuiya ya EAC imepiga hatua kubwa katika kuendeleza misingi ya utangamano,” Dkt Ruto akasema.

Uenyekiti wa Jumuiya ya EAC

Rais Ruto anachukua uenyekiti wa jumuiya hiyo wakati ambapo wanachama wake wote wanane wanaendeleza ajenda ya kubuni utangamano wa kisiasa.

Kando na hayo, rais wa Kenya alieleza kuwa Kenya itaendelea kutekeleza wajibu wake kama mshirika katika muungano wa kiuchumi.

“Ndoto ya Utangamano wa Kisiasa katika EAC ni safari ya kipekee ya kuunganisha eneo hili letu,” Rais Ruto akasema huku akitaja kuwa kuna changamoto ambazo lazima zikabiliwe ili kufikia lengo hilo.

Hata hivyo, Dkt Ruto alisema kuna manufaa makubwa katika umoja wa kisiasa baina ya mataifa manane wanachama wa EAC, kuliko changamoto.

“Sharti kujizatiti kufaidi kutokana manufaa yanayoletwa na hatua hii ili kujenga jumuiya ya EAC thabiti ambayo itawezesha kubuniwa kwa soko la pamoja barani Afrika,” akaeleza.

Rais Ruto aliahidi kuwa wakati wa hatamu yake kama mwanachama wa EAC, ataipa kipaumbele ajenda ya kuboresha maisha ya watu wa Afrika Mashariki.

Bidhaa zinazozalishwa

“Tutalenga kuimarisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa, kuendeleza mpango wa uongezaji wa thamani mazao ya shambani, tutaendeleza biashara miongoni mwa mataifa ya ukanda huu na kuimarisha uwekezaji,” akasema.

Rais Ruto aliongeza kuwa nguzo hizo ni muhimu katika kupiga jeki chumi za mataifa wanachama wa EAC, uzalishaji wa nafasi za ajira na kufikia malengo ya maendeleo katika ukanda huu.

Aidha, mwenyekiti huyo mpya wa jumuiya ya EAC alishauri kuwa mataifa wanachama yanafaa kuondoa vikwazo vya kibiashara.

“Sharti mataifa ya EAC yaondoe vikwazo kama vile ushuru wa juu kwa bidhaa zinazoingizwa katika nchi wanachama, tuimarishe miundo msingi na tulenge kuoanisha sheria mbalimbali za kibiashara,” Rais Ruto akaeleza.