Ruto awaalika wawekezaji kutoka Korea Kusini kuwekeza barani
NA PCS
SEOUL, KOREA KUSINI
RAIS William Ruto amehutubia kongamano kuu la kwanza kabisa baina ya Korea Kusini na nchi za bara la Afrika na kusisitiza jukumu muhimu ambalo nchi hiyo ya bara Asia inaweza kutekeleza kuleta mageuzi Afrika.
Rais Ruto alisema Afrika inalenga kunufaika kikamilifu kutokana na ushirikiano na wawekezaji kutoka Korea Kusini.
Lengo, alisema, ni kupata maarifa ya kutumia rasilimali za Afrika ipasavyo ili kubuni nafasi za kazi na kuchochea ukuaji wa kiuchumi.
Alieleza licha ya Afrika kujivunia utajiri mkubwa unaojumuisha vijana wenye nguvu na ujuzi, vipande tele vya ardhi kwa kilimo, hifadhi kubwa za nishati mbadala na rasilimali nyingi za madini, bado mataifa ya bara hili yanajikokota.
Alisema ushirikiano wa Afrika na Korea Kusini unaweka zingatio katika uimarishaji wa masuala ya utoshelevu wa chakula, sayansi na teknolojia, amani na usalama, pamoja na afya.
“Kongamano hili kuu linatambua umuhimu wa Afrika na Korea Kusini kushirikiana kwa lengo la kuafikia maendeleo katika pande zote. Kuna haja ya kuhakikisha viongozi wanaunga mkono ushirikiano huu mzuri na kuibuka na mikakati inayoweza kuzaa matunda,” akasema Dkt Ruto mnamo Jumanne.
Kongamano hilo lenye mada “Mustakabili Tunaojiwekea Pamoja: Ukuaji wa Pamoja, Uendelevu na Mshikamano”, liliandaliwa na Rais Yoon Suk Yeol katika ukumbi wa Korea International Exhibition Centre mjini Goyang.