Kimataifa

Rwanda yapiga hatua kuu kiteknolojia kutengeneza ‘smartphones’ Afrika

October 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na AFP

KIGALI, RWANDA

JUHUDI za Rwanda kuwa kitovu cha teknolojia barani Afrika zimepigwa jeki baada ya kampuni moja nchini humo inayomilikiwa na bwanyenye wa nchi hiyo ambaye pia ana asili ya India kuzindua simu mbili za kisasa ilizozitaja kama aina ya kwanza ya simu “Zilizotengenezewa Afrika.”

Aina hizo za simu – Mara X na Mara Z – zitatumia mfumo wa utendakazi wa Andorid ya Google na zitauzwa kwa Sh19,705 na Sh13,482 mtawalia.

Zitashindana na Samsung, ambayo simu yake ya bei ya chini zaidi huuzwa kwa Sh5,606 huku simu zisizokuwa na nembo zikiuzwa kwa Sh3,924.

Mkurugenzi wa Mara Group Ashish Thakkar, alisema kampuni yake ilikuwa ikilenga wateja walio tayari kulipia kiasi cha juu zaidi ili kupata thamani.

“Hii ndiyo kampuni ya kwanza ya kutengeneza simu za ‘smartphone’ Afrika,” Bw Thakkar alieleza vyombo vya habari baada ya kuzuru kampuni hiyo pamoja na Rais wa Rwanda Paul Kagame.

Kampuni hukusanya simu za smartphones Misri, Uhabeshi, Algeria na Afrika Kusini lakini zinaagizia nje vipuri vyake, alisema.

“Hakika sisi ndio wa kwanza tunaofanya uzalishaji. Tunaunda kifaa muhimu cha utendakazi (motherboard), tunaunda vijisehemu (sub boards) vyake katika mchakato huo wote. Kuna zaidi ya vijisehemu 1,000 kwa kila simu,” alisema.

Rais Kagame alisema anatumai simu hizo zitaongeza kiwango cha matumizi ya simu za Smartphone miongoni mwa Wanyarwanda ambacho kwa sasa kinakaribia asilimia 15.

“Wanyarwanda tayari wanatumia simu za ‘smartphones’ lakini tunataka kuwezesha wengine wengi. Kuanzishwa kwa simu za Mara kutawezesha umilisi wa simu za smartphones kuwafikia raia zaidi wa Rwanda,” alisema Kagame.

Kulingana na Thakkar, kiwanda hicho kilikuwa kimegharimu Sh2.5 billioni na kingeweza kuunda simu 1,200 kila siku.

Alisema kampuni ya Mara Group inatumai kupata faida kutokana na Mkataba wa Biashara Huru Barani Afrika, unaolenga kubuni kitengo cha kibiashara kinachojumuisha mataifa 55.

Mkataba huo utaanza kufanya kazi Julai 2020 ukilenga kuunganisha watu 1.3 bilioni na kuunda kitengo cha kiuchumi cha Sh353 trilioni.

Hata hivyo, mkataba huo ungali katika hatua za mwanzo kabisa na hakuna makataa yaliyoafikiwa kuhusu kufutilia mbali ushuru wa kibiashara baina ya mataifa.

 

Tafsiri: MARY WANGARI