• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Saba wafariki Nigeria wakipigania mchele

Saba wafariki Nigeria wakipigania mchele

NA MASHIRIKA

ABUJA, NIGERIA

WATU saba walifariki na wengine kujeruhiwa Nigeria kwenye mkanyagano waking’ang’ania mchele wa bei nafuu.

Vifo hivyo vilitangazwa na Shirika la Wateja Nigeria (NCS).

Haya yanajiri wakati nchi hiyo ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula huku bei ya bidhaa mbalimbali ikibaki kuwa juu.

Wiki iliyopita NCS iliahidi kusambaza vyakula mbalimbali madukani ili kusaidia kukabiliana na changamoto za sasa za utoshelevu wa chakula.

Shughuli hiyo ilianza Ijumaa wiki jana. Watu hao walikuwa waking’ang’ania bidhaa hiyo iliyokuwa ikiuzwa Sh925.96 kwa mfuko wa kilo 25.

Kwa kawaida, bidhaa hiyo huuzwa Sh3,709.11.

Lakini mambo yaliharibika baada ya wateja kujulishwa kwamba shughuli hiyo ya kuuza bidhaa hiyo ingerejea siku iliyofuata kutokana na uhaba.

“Kisa hicho kiliibuka tulipoishiwa na bidhaa hiyo na kutangaza kuendelea na shughuli hiyo siku iliyofuatia. Hii iliwakasirisha watu na kuwalazimisha kuanza kung’ang’ania bidhaa hiyo,” NCS ilisema katika taarifa.

Wakati huo huo, vyama vya wafanyikazi nchini humo jana vilianza maandamano ya siku mbili kupinga kuongezeka kwa gharama ya maisha.

Bei ya bidhaa mbalimbali nchini humo imepanda, jambo ambalo limewafanya wengi kutilia shaka utendakazi wa rais wa nchi hiyo Bola Tinubu.

Katika barua iliyosambazwa kwa umma kabla ya maandamano kuanza, NLC ilisema wanataka serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua za haraka kusuluhisha suala la kupanda kwa gharama ya maisha.

“Fungua maghala yote ya kuhifadhi chakula na uhakikishe usambazaji sawa nchini kote,” waandamanaji hao walisema.

Pia walitoa wito kwa serikali kuachana na sera za Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambazo wanaamini zinafanya gharama ya maisha kuwa juu zaidi.

Kabla ya maandamano hayo, Waziri wa Fedha wa Nigeria, Wale Edun alisema kwamba Rais Bola Tinubu “anasikiliza kwa makini na kuchukua hatua ili kukidhi mahitaji ya wananchi”.

Jumatatu, waziri huyo alitangaza kuwa serikali inapanga kutoa fedha ili kusaidia zaidi ya familia milioni 12 zilizo hatarini.

Edun aliwaomba Wanigeria wawe na subira wakati serikali ikijaribu kufufua uchumi wan chi hiyo.

“Rais anajaribu awezalo kuufufua uchumi wa nchi yetu. Hivyo tunawaomba wananchi waendelee kuwa na subira,” Bw Edun alisema.

Benki ya Maendeleo ya Afrika tayari hapo awali ilionya kuwa kupanda kwa gharama ya maisha huenda ikaleta machafuko na mgomo.

  • Tags

You can share this post!

Benki ya I&M yafungua tawi la Watamu

Simba Arati sasa amtetea Dkt Monda

T L