Sababu ya mwizi kurudisha saa aliyoiba miaka 20 iliyopita
Na MASHIRIKA
MICHIGAN, AMERIKA
MWIZI aliyeiba saa kutoka kituo cha treni miaka 20 iliyopita aliamua kuirudisha hivi majuzi.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, makavazi ya Ford ilipokea simu kutoka kwa mtu ambaye hakujitambulisha aliyesema anataka saa hiyo aliyokuwa ameiba kutoka kwa kituo cha treni cha Michigan Central “irudi nyumbani”.
Alieleza mahali ambako ataacha saa hiyo kubwa ya ukutani ambayo ni ya kihistoria ili maafisa watumwe huko kuichukua.
Ripoti zinasema saa iliyoibiwa ilikuwa mojawapo ya sura za kituo hicho kilichojengwa mwaka wa 1913 na kuhudumu hadi 1988 kilipofungwa.
Hata hivyo, kituo hicho sasa kimeanza kufanyiwa ukarabati na maafisa husika wanaamini mwizi huyo alitaka kuhisi kuhusika katika shughuli ya kukifufua upya.
“Tungependa kuomba mtu yeyote ambaye huenda ana chombo chochote cha kihistoria na anataka kukirudisha awasiliane nasi. Hatutauliza maswali yoyote,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika la Ford Land linalohusika katika ujenzi huo, Dave Dubensky.
-Imekusanywa na Valentine Obara