Kimataifa

Samia achemkia Muungano wa Ulaya; ataka Tanzania iachwe ijifanyie maamuzi yake

Na MASHIRIKA December 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

DAR-ES-SALAAM, TANZANIA

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekemea muungano wa Bara Ulaya akidai kuwa Tanzania ni nchi huru.

“Serikali hii haiwezi kuamrishwa. Sisi ni nchi huru,” rais huyo alisema.

Mbali na hayo, kiongozi huyo alishikilia kuwa vurugu za uchaguzi zilichochewa na watu wa ndani na nje ya nchi yake kwa lengo la kuibomoa serikali yake.

Kulingana na rais huyo, serikali yake ina uwezo na iko huru kukabiliana na changomoto zake ikiwemo machafuo na maandamano yaliyoshuhudiwa nchini humo baada ya uchaguzi.

Haya yanajiri huku kukiwa na fununu kuwa maandamano mengine yanapangwa kufanyika kati ya Disemba 9, 2025 na Disemba 25, 2025.

“Nataka niwaambie, wakati wowote wakija, tumejipanga,” alisema Rais Samia.

Rais Samia pia alisema kuwa wapo wanaoishinikiza serikali “imwachie mtu fulani uongozi” kama sharti la maridhiano, jambo alilokataa akisema maridhiano hayataongozwa kwa mashinikizo kutoka nje.

Ameongeza kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kilishinda uchaguzi kwa asilimia 97, na kwamba wanaouliza kwa nini asilimia hiyo ni kubwa “hawakuwepo kwenye uchaguzi,” hivyo hawapaswi kutilia shaka maamuzi ya waliojitokeza kupiga kura.

Amesisitiza kuwa pamoja na jeraha lililotokana na vurugu zilizopita, Watanzania wenyewe ndiyo watakaoliokoa nchi yao kupitia majukwaa ya mazungumzo, ushirikiano wa wazee, na kuwaongoza vijana kutojiingiza kwenye mipango ya kuchochewa na watu ambao hakuwataja.

“Tukae tuzungumze. Wazee wetu na vijana wetu wasitumike. Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe na sio watu wa nje.”

Siku chache zilizopita, Bunge la Ulaya lilipendekeza kusitisha ufadhili wake kwa nchi ya Tanzania kufuatia vurugu vya baada ya uchaguzi.

Kulingana na bunge hilo, maelfu waliuawa na wengine kujeruhiwa nchini humo.

Katika azimio lililopitishwa Novemba 27 kwa kura 539 wabunge waliitaka Tume ya Ulaya kusitisha msaada wowote wa moja kwa moja kwa mamlaka ya Tanzania.

Serikali ya Samia imekuwa kwenye rada huku baadhi ya viongozi duniani wakimkemea rais huyo kufuatia vifo vya mamia na utekaji nyara.

Wiki jana Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilipokea ombi la kuichunguza serikali ya Tanzania kuhusu madai ya ghasia na mauaji wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Chama cha Wanasheria wa Madrid, pamoja na mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu, yanamtaka mwendesha mashtaka wa ICC kufungua uchunguzi rasmi kuhusu kile wanachokirejelea kuwa ni shambulio la kiserikali dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na mauaji, kuangamiza, kutesa na kuwateka nyara watu wasio na hatia.

Utawala wa Bi Suluhu pia unahisi shinikizo kwani Kamati ya Seneti ya Mahusiano ya Kigeni ya Amerika imetaka kufanywa kwa uchunguzi huru na wa haraka kuhusu mauaji ya raia yaliyofanywa na maafisa wa usalama nchini humo.