Kimataifa

Samia pazuri kutwaa urais Tanzania bila upinzani wowote

Na REUTERS August 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

DAR ES SALAAM, TANZANIA

TUME ya Uchaguzi Tanzania (INEC) mnamo Jumatano ilimzuia mwaniaji wa urais wa chama cha pili kwa ukubwa katika upinzani kushiriki kura kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Hatua hii sasa inamwacha Rais Samia Suluhu na wakati rahisi kushinda kura hiyo kwa sababu atakuwa akimenyana tu na wapinzani kutoka vyama vidogo vidogo.

Suluhu na mgombeaji mwenza wake Emmanuel Nchimbi waliidhinishwa kuwania kura hiyo ya Oktoba 29, 2025.

Uchaguzi huo utaandaliwa bila chama kikubwa cha upinzani Chadema kushiriki.

Chadema mnamo Aprili iliondolewa baada ya kukataa kutia saini mwongozo wa kuendesha uchaguzi huo wakati huo chama hicho kikiwa kinapigania mageuzi kwenye sheria za kura.

Jumatano, INEC ilikataa kupokea karatasi za uteuzi kutoka kwa Luhaga Mpina wa chama cha ACT Wazalendo, ambacho ni cha pili kwa ukubwa katika upinzani baada ya Chadema.

Awali Jumanne, Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa ilimpiga marufuku Mpina ikitaja malalamishi kutoka kwa wanachama wa chama chake waliodai ACT Wazalendo haikufuata utaratibu kwenye mchujo.

Mpina amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali na alikuwa amehama chama tawala cha CCM awali mwezi huu.

“Uamuzi huo ni aibu na unaibua maswali kuhusu uwazi kwenye uchaguzi na iwapo tume yenyewe inaendesha kazi yake kwa njia huru,” akasema Ado Shaibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo.

Suluhu anawania urais kwa mara ya kwanza baada ya kuingia afisini mnamo 2021 kutokana na mauti ya aliyekuwa Rais John Pombe Magufuli.

Uteuzi wa wanaoshiriki uchaguzi ulitamatika Jumatano na sasa Suluhu na wapinzani wake ‘wadogo’ wataendeleza kampeni kali ya kuingia ikulu.