Kimataifa

Serikali Ethiopia yatoa makataa ya saa 72 kwa wapiganaji wa Tigray wajisalimishe

November 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

ADDIS ABABA, Ethiopia

WAZIRI Mkuu wa Ethiopia ametoa makataa ya saa 72 kwa wapiganaji eneo la Tigray kujisalimisha huku wanajeshi wakielekea katika mji mkuu wa eneo hilo la Kaskazini, Mekelle.

Abiy Ahmed aliwaambia viongozi wa Tigray kwamba serikali yake haitakoma kushambulia wapiganaji wao.

Lakini kundi la Tigray People’s Liberation Front (TPLF), linalodhibiti eneo hilo lenye milima, limesisitiza kuendelea na vita.

Mamia ya watu wameripotiwa kufariki na wengine kupoteza makao katika mapigano kati ya wafuasi wa TPLF na wanajeshi wa serikali.

Umoja wa Mataifa (UN) imeonya kuwa mapigano hayo huenda yakasababisha mgogoro wa kibinadamu katika eneo hilo na nchini Ethiopia kwa ujumla.

Awali, wanajeshi wa Ethiopia walionya kuwa wakazi 500,000 wa jiji wa Mekelle kwa watazingira eneo hilo na kufanya mashambulio makali.

“Hamna atakayeonewa huruma,” msemaji wa poliisi akasema.

Kiongozi wa TPLF Debretsion Gebremichael aliwaambia wanahabari kwamba wapiganaji wake wamefaulu kuwadhibiti wanajeshi wa serikali.

“Wanatuma makundi ya wanajeshi lakini wameshindwa,” akawaambia wanahabari wa shirika la habari la Reuters.

Serikali ilisema kuwa wanajeshi wake walitwaa udhibiti wa miji mikuu wiki jana.

Lakini habari hizo haziwezi kuthibitishwa kwa sababu tangu mapigano hayo yaanze, mawasiliano ya simu na huduma za Intaneti zilikatizwa.

Katika taarifa aliyoitoa Jumapili aliyolengwa ifikie uongozi wa TPLF, Waziri Mkuu Abiy alisema: “Safari yenu ya uharibifu itakoma, na tunawahimiza kujisalimisha kwa amani. Hii ni kwa sababu baada ya saa 72 tutazima kabisa. Mtumie muda huu tulioutoa.”

Kiongozi huyo alisema wanapigaji wa TPLF wanapasa kujisalimisha kwa amani na wakazi wa Mekelle waunge mkono wanajeshi wa serikali katika kuhakikisha kuwa wafuasi wa “kundi hili wanaadhibiwa.”