Kimataifa

Serikali Lebanon yajiuzulu kutokana na presha kutoka kwa waandamanaji

August 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

BEIRUT, LEBANON

SERIKALI ya Lebanon Jumatatu, Agosti 10, 2020, imejiuzulu kutokana na ongezeko la kero kutoka wa umma kufuatia mlipuko uliotokea Jumanne wiki jana jijini Beirut ambapo zaidi ya watu 200 walifariki huku wengine zaidi ya 6,000 wakijeruhiwa.

Mlipuko huo ambao ulitokea ndani ya ghala moja ambapo kemikali aina ya ammonium nitrate ilikuwa imehifadhiwa pia ulisababisha uharibifu wa mali ya thamani kubwa katika jiji hilo.

Tangazo la kujiuzulu kwa serikali hiyo lilipeperushwa moja kwa moja kupitia runinga ya kitaifa majira ya jioni ambapo Waziri Mkuu Hassan Diab alitangaza hilo bayana.

Watu wengine wamewasuta viongozi wa serikali ya Lebanon wakidai mkasa huo ulichangiwa na mapuuza yao pamoja na ufisadi.

Raia wamekuwa wakiandamana katika barabara za Beirut kwa siku mbili mfululizo wakilaani kutokea kwa mkasa huo.

“Leo, tunafuata matakwa ya wananchi ambao wametaka uwajibikaji kufuatia mkasa huo uliosababishwa na kemikali ambayo imefichwa kwa miaka saba. Pia tunazingatia haja yao ya kutaka mabadiliko. Katika hali kama hii, ninatangaza kujiuzulu kwa serikali,” akasema Waziri Mkuu Diab.

Baraza la Mawaziri la nchi hiyo liliundwa mnamo Januari 2020 kupitia uungwaji mkono kutoka kwa kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.

Duru zilisema kuwa mawaziri hao walikutana Jumatatu, Agosti 10, 2020, asubuhi na kupendekeza kuwa wajiuzulu.