Kimataifa

Serikali ya Tanzania yaharamisha maandamano ya Jumanne Desemba 9

Na REUTERS December 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

DAR ES SALAAM, TANZANIA

POLISI nchini Tanzania wamesema Ijumaa kwamba maandamano yanayotarajiwa kufanyika nchini kote wiki ijayo yatakuwa haramu, jambo linaloweza kupelekea ghasia mpya baada ya watu ambao idadi yao haikubainika kupoteza maisha katika maandamano ya uchaguzi mwezi uliopita.

Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi kwa uchaguzi wa Oktoba baada ya wapinzani wake wakuu kupigwa marufuku kushiriki, jambo lililosababisha maandamano yaliyochochewa kwa sehemu na kile ambacho wanaharakati walisema ni ukandamizaji wa upinzani.

Vikundi vya haki za binadamu, vyama vya upinzani na Umoja wa Mataifa vimesema kuwa mamia ya watu wanaweza kuwa wameuawa katika mapigano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama.

Serikali inakana kuzima upinzani na inapinga takwimu hizo ikisema zimeongezwa chumvi.

Msemaji wa polisi David Misime, alisema kuwa bado hawajapokea taarifa rasmi kutoka kwa yeyote anayetaka kuandaa maandamano, baada ya machapisho katika mitandao ya kijamii kusambaza wito wa maandamano ya Desemba 9.

“Jeshi la Polisi linakataza maandamano haya, ambayo yamepewa jina la ‘maandamano yasiyo na kikomo na ya amani’, yafanyike,” alisema katika taarifa.

Misime alisema wale wanaopanga maandamano wanawahimiza washiriki, miongoni mwa mambo mengine, kuharibu mali, kuvuruga huduma katika hospitali na kubaki barabarani kwa muda usio na kikomo ili kuathiri shughuli za kiuchumi.

Alhamisi, kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu kilihimiza mamlaka za Tanzania na vikosi vya usalama kulinda haki ya wananchi kuungana na kuzuia ukiukaji wowote zaidi kabla ya maandamano yaliyopangwa.

Rais Hassan ameahidi kuchunguza ghasia za uchaguzi na ametoa rambirambi kwa familia zilizoathirika, jambo ambalo ni kuthibitisha hadharani mara ya kwanza vurugu hizo, ambazo zimepelekea mgogoro mkubwa wa kisiasa katika nchi kwa miongo kadhaa.

“Tunasikia kuna mengine yanayopangwa, wakija, tuko tayari,” Hassan alisema kwenye mkutano jijini Dar es Salaam Jumanne, akirejelea maandamano yanayopangwa.

Amerika ilisema Alhamisi kuwa inachunguza uhusiano wake na Tanzania kutokana na wasiwasi kuhusu uhuru wa dini, uhuru wa kujieleza, vikwazo kwa uwekezaji na ghasia dhidi ya raia.

Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Tanzania ilisema Ijumaa kuwa inachukulia kwa makini taarifa tofauti kutoka kwa ujumbe wa Muungano wa Ulaya, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na baadhi ya nchi zikiwemo Amerikaz, Ghana, Ubelgiji, Canada na Denmark.