Kimataifa

Serikali yatetea hatua ya kuajiri wateteza wa kuboresha uhusiano na Trump

Na MWANDISHI WETU August 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI ya William Ruto imetetea hatua yake ya kuajiri watetezi jijini Washington D.C kusaidia kuimarisha uhusiano na serikali ya Rais Donald Trump.

Kwenye taarifa iliyoandikwa na Kinara wa Mawaziri aliye pia Waziri wa Mashauri ya Kigeni Musalia Mudavadi, serikali inasema ni jambo la kawaida kwa mataifa kuajiri watetezi, maarufu kwa Kiingereza kama ‘Lobbyists’ kutengeneza mahusiano na serikali ya Amerika.

Alisema mahusiano mazuri husaidia nchi katika nyanja za kibiashara, kiusalama na kidiplomasia, ikimaanisha kwamba wananchi wote ndio wanafaidika.

“Kufanya kazi kwetu na makundi haya ya watetezi huwa kumeongozwa na maslahi ya nchi na hufanywa kwa kuzingatia kikamilifu sheria za Kenya,” akasema Bw Mudavadi.

Bw Mudavadi alikuwa anarejelea taarifa ya kipekee iliyochapishwa na Daily Nation na Taifa Leo kuhusu jinsi serikali ya Ruto imetumia mamia ya mamilioni ya pesa za walipa ushuru, kulipa watetezi ili kumwonyesha Rais kwa mwangaza mzuri mbele ya serikali ya Trump.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kwamba sio Ruto pekee aliyetumia mamilioni hayo ila wamezeaji wa kiti cha urais walio upinzani kwa sasa, kama Jimi Wanjigi na Fred Matiang’i pia wameajiri watetezi wa kusaidia kuvutia utawala wa Trump upande wao, kiini kikiaminika kuwa uchaguzi mkuu ujao wa 2027.

SOMA ZAIDI: Ruto, Upinzani watumia hadi Sh1 bilioni kumweka Trump ‘mpangoni’ kwa kura 2027