Sherehe Liberia baada ya Trump kusifia Rais wao kwa Kiingereza safi
MONROVIA, LIBERIA
RAIA wa Liberia mnamo Alhamisi walisherehekea baada ya Rais Donald Trump wa Amerika kumsifia rais wao Joseph Boakai kwa kuzungumza Kiingereza kwa ufasaha katika kikao cha biashara na uwekezaji kwenye Ikulu ya White House.
Trump alishangaa jinsi Boakai alilonga Kiingereza kwenye kikao hicho ambacho kilishirikisha pia marais wa Guinea Bissau, Mauritania, Senegal na Gabon.
Mkutano huo ulikuwa wa kujadili jinsi mataifa hayo ya Afrika magharibi yangeimarisha chumi zao na uwekezaji baina yao na Amerika.
Baadhi ya raia wa Liberia katika jiji kuu la Monrovia walisema ziara ya Ikulu na sifa za Trump kwa kiongozi wao zimeongezea nchi yao sifa machoni mwa ulimwengu.
“Jinsi rais wetu Boakai alizungumza kwa umilisi ni wazi alikuwa na msingi imara wa elimu yake hapa Liberia. Hotuba yake ilifafanua jinsi anataka tunufaike kutokana na uhusiano wetu na Amerika,” akasema mwanahabari wa redio Augustus Kaine.
Magazeti yote Liberia yalichapisha kauli za Trump kama habari kuu Ijumaa.
“Boakai amewasilisha matakwa ya Liberia kwa ushujaa na umakinifu na amevutia wenyeji wake,” ilisoma taarifa kuu ya habari katika gazeti moja la nchi hiyo.
Habari kuu katika gazeti lingine zilisema ‘Liberia yapata alama zote katika mwaliko wa Trump’ huku taarifa hizo zikisisitiza Amerika si taifa dogo katika nyanja zote.
Akiongea katika kikao cha White House, Boakai alialika Amerika kusaidia nchi yake, nayo inufaike na utajiri wa madini yaliyomo Liberia.
Pia alipigia debe nchi yake kama yenye demokrasia Afrika akisema chaguzi zake huwa huru na mwamuzi ni raia.
Kingereza ni lugha rasmi Liberia – taifa ambalo Waamerika weusi walikuwa wakoloni wake kuanzia 1822 lilipoanzishwa