Sina hakika, Trump sasa asema kuhusu ufanisi wa sera zake
WASHINGTON DC, AMERIKA
RAIS Donald Trump ameelezea wasiwasi kuhusu iwapo chama tawala cha Republican kitadumisha udhibiti wa bunge kwenye chaguzi za muhula wa kati mwaka ujao kwa sababu baadhi ya sera zake kiuchumi bado hazijatekelezwa kikamilifu, shirika la Wall Street Journal liliripoti Jumamosi.
Trump, kwenye mahojiano Ijumaa, alieleza shirika hilo, “siwezi nikawaeleza. Sijui ni lini hela zote hizi zitaanza kuwa na matokeo halisi,” alipoulizwa kuhusu iwapo Republican itapoteza bunge Novemba.
Ikulu haikujibu mara moja ombi la Reuters la kuzungumzia suala hilo.
Rais amehoji kuwa sera zake za kiuchumi, ikiwemo hatua yake ya kuanzisha msururu wa ada za ushuru kwa bidhaa zinazoingizwa nchini, zinaunda kazi, kupiga jeki soko la hisa na kuvutia uwekezaji Amerika.
Baada ya kufanya kampeni mwaka jana kwa ahadi za kudhibiti mfumuko wa bei, Trump katika majuma machache yaliyopita amebadilisha kauli na kupuuzilia mbali matatizo yanayohusu bei ya bidhaa kuwa uongo, akimlaumu aliyekuwa rais Joe Biden kuyahusu na kuahidi sera zake kiuchumi zitanufaisha raia wa Amerika mwaka ujao.
“Nafikiri kufikia wakati tutalazimika kuzungumza kuhusu uchaguzi, katika muda wa miezi michache ijayo, nafikiri bei zetu zitakuwa katika hali shwari,” alisema Trump kwenye mahojiano.
Mwezi uliopita, rais alipunguza ada za ushuru kwa bidhaa zaidi ya 200 za chakula kufuatia kutoridhika kunakozidi kuongezeka miongoni mwa wateja Waamerika kuhusu bei ghali ya bidhaa za chakula.
Rais hakusema iwapo atapunguza ushuru kwa bidhaa za ziada, ilisema WSJ. Kiwango cha kumkubali Trump kwa jumla kilipanda hadi asilimia 41 katika kura mpya ya maoni iliyoendeshwa na Reuters/Ipsos lakini kiwango cha kukubali utendakazi wake kuhusu gharama ya maisha kilikuwa asilimia 31 pekee.
Wanasiasa wa Democrat wamenyakua misururu ya ushindi kwenye chaguzi za majimbo na majiji nchini ikiwemo Virginia, New Jersey na New York City, ambapo wasiwasi wa wapiga kura kuhusu uwezo wa ununuzi pamoja na bei ghali za bidhaa za chakula, zilikuwa masuala makuu.
Maafisa wamesema Trump atajitosa barabarani mwaka ujao kuwafanyia kampeni wagombea wa Republican na kusisitiza ufanisi wa sera zake kiuchumi.
Trump amesema hatua yake ya kupunguza ada na ushuru unaotozwa bidhaa za kigeni utaongeza pesa kwenye mifuko ya familia za Amerika.