Soko la Pamoja la Afrika: Makubaliano yaafikiwa
Na AFP
MUUNGANO wa Afrika (AU) mnamo Jumapili uliafikia maelewano ya kibiashara ambayo yatawezesha biashara baina ya mataifa ya bara hili kufanyika bila vizuizi.
Hatua hii imeafikiwa baada ya miaka 17 ya majadiliano ya kutafuta muafaka kuhusu suala hilo.
Katika kongamano la siku mbili lililoandaliwa jijini Niamey, Niger, iliafikiwa kuwa mataifa ya Afrika mbali na kuondoa vizuizi vya kibiashara, yatakuwa na mfumo sawa wa kidijitali wa malipo utakaotumiwa barani kote.
Maelewano hayo yamekuwa yakisubiriwa kwa muda mrefu, na hatua ya Nigeria na Benin kuyatia sahihi Jumapili iliyapa nguvu.
Hadi sasa mataifa 54 kati ya 55 barani yakiwa yameafikiana kuhusu maelewano hayo.
Ni Eritrea pekee kati ya mataifa wanachama wa AU ambayo haijatia sahihi, na ilisema inawaza kufanya hivyo.
AU ilizindua awamu ya kuanza kuweka mfumo wa kibiashara utakaoanza Julai 1, 2020.
Mwenyekiti wa Muungano wa AU, Moussa Faki alitaja hatua hiyo kuwa ya kihistoria baada ya miaka mingi ya kutafuta maelewano.
“Ndoto ya zamani inaanza kuafikiwa, lazima mababa zetu wamefurahi sasa. Hili litakuwa eneo kubwa zaidi kibiashara duniani,” akasema Faki.
Takriban wajumbe 4,500, wakiwemo Marais 32 na zaidi ya mawaziri 100 walihudhuria kongamano hilo.
Sahihi
Maelewano hayo yalifanywa rasmi Aprili 2019 wakati mataifa ya AU yalitia sahihi.
Rais wa Niger, Mahamadou Issoufou alisifu hatua hiyo kuwa kubwa zaidi barani humu kwa takriban miaka 60 sasa.
“Hii ndiyo hatua kubwa sana bara la Afrika limepiga tangu Muungano wa Umoja wa Afrika (OAU) ulipoanzishwa mnamo 1963,” akasema Issoufou.
Kulingana na maelewano hayo, katika muda wa miaka mitano, ambao ndio muda utakaotumika kutekeleza mfumo huo kikamilifu, vizuizi vya kibiashara baina ya mataifa ya Afrika vitakuwa vimepunguzwa, na ushuru wa miapkani kuondolewa kwa asilimia 90.
Mataifa ya chini kimapato, hata hivyo, yatapewa muda zaidi kabla ya kuondoa ushuru kwa bidhaa zinazoingizwa katika mipaka yao, yakipewa kati ya miaka 10 na 15.
AU inasema kuwa mfumo huo utainua biashara barani kwa asilimia 60 kufikia 2022.
Kwa sasa, mataifa ya Afrika hufanya biashara kwa asilimia 16 ya bidhaa zinazozalishwa barani, ikilinganishwa na asilimia 65 katika mataifa ya bara Uropa.
Suala la usalama nalo litakuwa miongoni mwa mambo yanayolenga kusuluhishwa katika maelewano hayo, wakati mataifa kadha yanapokumbwa na tatizo la mavamizi ya kigaidi na machafuko ya kisiasa.