• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Spika wa Bunge ajiuzulu akitarajia kunyakwa wakati wowote kwa tuhuma za ufisadi

Spika wa Bunge ajiuzulu akitarajia kunyakwa wakati wowote kwa tuhuma za ufisadi

JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

NA MASHIRIKA

SPIKA wa Bunge la Afrika Kusini Bi Nosiviwe Mapisa-Nqakula alijiuzulu wadhifa wake baada ya kupoteza ombi la kuzuia kukamatwa kwake kutokana na tuhuma za ufisadi.

Siku ya Jumatano, polisi walifika nyumbani kwake kufanya upelelezi, ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa rushwa unaomkabili. Hata hivyo, hawakutoa maelezo kuhusu uchunguzi huo wala madai hayo.

Bi Mapisa-Nqakula,67, anatuhumiwa kuitisha hongo ili kupeana kandarasi wakati alipokuwa waziri wa ulinzi.

Bi Mapisa-Nqakula anakabiliwa na madai kadhaa ya kuomba hongo ya kiasi cha Sh15.6 milioni kutoka kwa mmiliki wa kampuni moja nchini humo ili kupata zabuni ya kusafirisha vifaa vya jeshi nchini Afrika Kusini kutoka mataifa mengine.

Mwanaharakati huyo mkongwe wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi aliteuliwa kuwa spika mwaka wa 2021.

Kabla ya hapo, alihudumu kama waziri wa ulinzi kwa miaka saba.

Bi Mapisa-Nqakula alikana madai hayo, akitaja kuwa kujiuzulu kwake hakumaanishi kukubali kuwa na hatia.

Kulingana naye, mashtaka hayo yana uzito na hawezi kuendelea na jukumu hilo.

Kujiuzulu huko, kunaanza kutekelezwa mara moja, ikiambatana na kuacha kazi kama mbunge.

Wiki iliyopita, mawakili wa Mapisa-Nqakula waliwasilisha ombi la kuzuia kukamatwa, wakisema ingevunjia heshima yake.

Jumanne, mahakama yalikataa ombi hilo, kwa msingi kwamba suala hilo halikuwa la dharura na hayakuweza kukisia juu ya kukamatwa ambako bado hakujafanyika.

Kujiuzulu kwake kunajiri kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi ujao, ambao baadhi wanaamini unaweza kuwa mgumu kwa chama tawala cha African National Congress (ANC).

Chama hicho ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 1994, kimekuwa kikikabiliwa na tuhuma za mara kwa mara za rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma, jambo ambalo limekuwa suala kuu la uchaguzi.

  • Tags

You can share this post!

Mkulima aliyechanganya maparachichi ndani ya shamba la chai...

Mambo ni unyo unyo ‘Ndovu’ Arsenal ikikanyaga...

T L