Kimataifa

Sudan yaanza mazungumzo huku ikizidisha juhudi iondolewe katika orodha mbaya

October 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na AFP

KHARTOUM, Sudan

BARAZA linalotawala Sudan na viongozi wa waasi wameanzisha mazungumzo kuhusu amani jana Jumatatu kwa lengo la kukomesha ghasia nchini humo, mojawapo ya masharti muhimu ikiwa ni kuondolewa katika orodha mbaya ya wafadhili wa magaidi ya Amerika.

Imeripotiwa kuwa, baraza hilo ambalo ni serikali ya mpito, limepatia kipaumbele suala la amani na waasi wanaopigana Khartoum.

Kuorodheshwa kama taifa linalofadhili ugaidi kunaizuia kabisa Sudan kuondolewa mzigo wa deni na kupata ufadhili muhimu wa kifedha kutoka kwa wakopeshaji kama vile Hazina ya Fedha Kimataifa na Benki ya Ulimwengu.

Kuondolewa katika orodha hiyo kutawezesha kufungua milango ya uwekezaji wa kigeni.

Alipowasili Juba Jumatatu, Mohamed Hamdan Dagalo, mwanachama wa baraza kuu, na kiongozi wa kikosi cha jeshi la Rapid Support Forces, alielezea matumaini.

“Tutaanza majadiliano kwa mioyo mikunjufu na tunamaanisha kuhusu kuleta amani Sudan,” alisema Dagalo almaarufu Hemedti.

Baraza hilo lilichukua usukani wa serikali mnamo Agosti wakati vikosi vya jeshi na makundi ya raia na waandamanaji walipotia sahihi mkataba wa ugavi wa mamlaka wa miaka mitatu, baada ya miezi kadha ya machafuko baada ya kung’olewa kwa Rais Omar al-Bashir mnamo Aprili.

Sudan Kusini iliwaleta pamoja wanachama wa baraza na viongozi wa waasi kutoka maeneo kadha kwa majadiliano mapya.

Maelfu ya watu wameuawa katika vita vya kikabila Sudan, ikiwemo ghasia katika eneo la Magharibi mwa Darfur, ambapo waasi wamekuwa wakipigana na serikali tangu 2003.

Mnamo Agosti, maafisa wa Sudan na waasi waliandaa shughuli ya mazungumzo ya miezi miwili kuanzia Oktoba 14.

“Huu unapaswa kuwa mchakato wa mwisho wa mazungumzo yatakayoangazia kiini cha vita na ubaguzi. Tumepania kuwa 2020 utakuwa mwaka wa amani Sudan,” alisema Yasir Arman, naibu mwenyekiti wa kundi la waasi la Sudan People’s Liberation Army-North (SPLM-North).